Popular services

TUME YA UCHAGUZI: MAKUNDI MAALUM NI SEHEMU YA MCHAKATO WA KIDEMOKRASIA, KURA YA MAPEMA IPO.


Na Nishan Khamis, Gamba — Alhamisi, Septemba 4, 2025.

Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini A leo imefanya kikao na wadau wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi Maalum ya mwaka 2015 iliyotungwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

Akifungua kikao hicho, Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini A, Jaala Makame Haji, alisema sera hiyo inalenga kuhakikisha makundi maalum yakiwemo watu wenye ulemavu, wanawake na vijana wanashirikishwa ipasavyo katika mchakato wa uchaguzi, kwani kufanya hivyo ni utekelezaji wa haki ya kikatiba.

Ameeleza kuwa tume katika ngazi ya wilaya tayari imetekeleza shughuli mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi, ambapo kura ya mapema imepangwa kufanyika Oktoba 28 na 29, kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha Sheria ya Uchaguzi kinachoeleza uhalali wa kura ya mapema. Aidha, aliwasihi washiriki wa kikao hicho kuwa mabalozi wa kutoa elimu ya uraia kwa jamii ili uchaguzi uwe na amani na utulivu.

Kwa upande wake, Subira Yussuf Shaaban, Msaidizi wa Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo, akiwasilisha mada mbalimbali, alisema ZEC itaendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa mujibu wa kanuni na sheria. Alibainisha kuwa huu utakuwa ni uchaguzi wa saba tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, ambapo utahusisha Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

Amesisitiza kuwa maeneo yasiyoruhusiwa kubandikwa picha za kampeni za wagombea ni pamoja na majengo ya taasisi za serikali, vyombo vya usafiri vya serikali, vituo vya maji, umeme na huduma nyingine za serikali, pamoja na nyumba binafsi ambazo hazijaruhusiwa na wamiliki wake. Aliitaka jamii kuzingatia na kufuata kanuni na sheria za uchaguzi ili kuepuka makosa yatakayoweza kuwaletea hatia.

Naye, Ali Vuai Ali, mwakilishi wa watu wenye ulemavu aliyehudhuria kikao hicho, alishukuru kwa ushirikishwaji wao na kupewa kipaumbele, akisema jambo hilo litawahamasisha kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi. Aliahidi kuwa wao kama kundi maalum watakuwa mabalozi wa kuhubiri amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.