Na Nishan Khamis, Zanzibar.
Kuna simulizi za wanawake waliopambana kimya kimya ndani ya jamii zao, na kuna simulizi za wanawake waliothubutu kuibuka hadharani na kupaza sauti kwa ajili ya wanyonge. Katika safu ya pili ndipo jina la Mama Mwaduwa Ali Khamis linapochomoza, mwanamke wa kijiji cha Raha Bumbwini wilaya ya Kaskazini B mkoa wa Kaskazini Unguja, mwenye historia ya ujasiri, uvumilivu na dhamira ya kweli ya kutetea jamii yake.Mama huyu si kiongozi wa kawaida ni mama wa watoto watano, wote wa kiume, aliyebeba jukumu la kulea, kufundisha na kusimama kama nguzo ya familia. Lakini zaidi ya hapo, ni sauti ya wanawake, vijana na wazee wa Bumbwini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipitia changamoto za kijamii na kiuchumi bila mtetezi wa karibu.
Mwadua alizaliwa tarehe 25 Novemba 1967 na kupata elimu ya msingi katika Skuli ya Bumbwini Misufini. Elimu yake iliishia darasa la saba, lakini maisha ya kijamii na mafunzo ya maisha halisi yakawa kitabu kikubwa cha kumbukumbu kwake. Alijiunga na CUF mwaka 1995 na alijitosa kwenye siasa kwa msukumo wa kuona mateso ya wanawake, vijana na wazee yakipuuzwa.
Mwaka 1995 alijaribu kugombea Uwakilishi kupitia CUF, lakini hakufanikiwa kutokana na ukandamizaji na ubaguzi wa kiuongozi ndani ya chama hicho. Tukio hilo lilimpa funzo kuwa siasa ni uwanja wa mapambano unaohitaji uvumilivu na msimamo.
Mwaka 2006, baada ya ushawishi wa rafiki yake wa karibu Bi Rufea Vuai na kufuatwa mara kwa mara na viongozi wa CCM, Mama Mwadua aliamua kujiunga na chama hicho. Hata hivyo, hakudumu kwa sababu hakuridhishwa na mwenendo wa mambo ndani ya chama. Baada ya hapo, mwaka 2009 alijiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jimbo. Mwaka 2010 aligombea Ubunge wa Jimbo la Bumbwini kupitia CHADEMA, lakini hakuibuka mshindi kutokana na nguvu kubwa ya CCM.
Licha ya changamoto hizo, wananchi wake walionesha kiu ya kumuona akiongoza, jambo lililomzidishia imani. Hata hivyo, tofauti za kisiasa na matatizo ya ruzuku ndani ya CHADEMA vilimfanya kuachana nacho mwaka 2025. Katika mwaka huohuo, Mama Mwadua aliamua kujiunga na CHAUMMA, chama anachoamini ndicho jukwaa sahihi la kuwatetea wananchi wa Bumbwini.
Kupitia CHAUMMA, sasa ni mgombea Ubunge wa Jimbo la Bumbwini. Ndoto yake ni kuona jamii yake inakombolewa dhidi ya changamoto sugu zinazowakumba wananchi wake. Anasisitiza kuwa akipata nafasi ya kuongoza, atapambana na changamoto za ardhi, ajira, udhalilishaji wa wanawake na vijana, pamoja na kuliwezesha jimbo kwa miradi ya maendeleo.
Mama Mwadua anaamini kuwa siasa si jukwaa la kunufaisha mtu binafsi, bali ni chombo cha kuwahudumia wananchi. Alisema katika viongozi wanaomvutia zaidi ni marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye kwake ni mfano wa uadilifu na kioo cha uongozi bora.
Katika safari yake ya kisiasa, Mama Mwadua ameshika nafasi muhimu ambazo zimemjenga kisiasa na kijamii, zikiwemo Mwenyekiti wa Jimbo kupitia CHADEMA mwaka 2009, Mwenyekiti wa BAWACHA Wilaya mwaka 2025, na Kiongozi wa Ngome ya Wanawake CHAUMMA Mkoa wa Kaskazini Unguja mwaka 2025. Kupitia nafasi hizi, amejijengea uzoefu na kuimarisha mtandao wake wa kisiasa.
Mbali na siasa, Mama Mwadua ni mjasiriamali mdogo anajishughulisha na biashara ya kuuza chapati na kilimo cha mazao mbalimbali, jambo linalomsaidia kujitegemea kiuchumi. Anasema changamoto za kifedha mara nyingi zimekuwa zikimrudisha nyuma, lakini hajawahi kukata tamaa kwani anaamini uchumi imara ni nguzo ya mwanasiasa jasiri.
Familia na jamii yake wamempa nguvu kubwa. Bi Rufea Vuai, mama mdogo wake, amekuwa naye bega kwa bega tangu mwanzo wa safari yake ya kisiasa. Vilevile, mtoto wake Mohamed Juma Khamis amekuwa chanzo cha matumaini, akimpa faraja kwa kumhakikishia siku moja atafanikiwa kuwa mwanasiasa wa mfano. Majirani kama Mwajuma Rashid pia wanamshuhudia kama mwanamke anayejitoa kwa dhati kuipigania Bumbwini.
Kwa sasa Mama Mwadua ni mjane baada ya kutalikiana na mumewe, lakini hali hiyo haijamkatisha tamaa. Kinyume chake, imeongeza dhamira yake ya kusimama imara kwa ajili ya familia yake na jamii nzima ya Bumbwini. Ana shauku kubwa ya kuikomboa Bumbwini kimaendeleo na kuacha alama kama mwanamke kiongozi wa mfano nchini.
Kwa wananchi wa Bumbwini, Mama Mwadua ni tumaini jipya,mwanamke shupavu anayelenga siasa zenye maono, utu na mabadiliko ya kwe

