Popular services

WAISLAMU WATAKIWA KUYAISHI MALEKEZO YA MTUME (S.A.W) KWA VITENDO

 WAISLAMU WATAKIWA KUYAISHI MALEKEZO YA MTUME (S.A.W) KWA VITENDO

NA FAUZIA MUSSA 

Katika mwezi huu mtukufu ambao Waislamu duniani kote wanakumbuka kuzaliwa kwa Mtume, Muhammad (S.A.W), wito umetolewa kwa waumini kuenzi maisha yake kwa matendo mema na kujiepusha na maovu, kama alivyoelekeza mwenyewe kwa mfano wa maisha yake bora.


Akizungumza wakati wa zoezi la usafi na uchangiaji damu lililofanyika madrasa ya Swiffat Nabawiyatul-Kareem, katika shamra shamra  za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume na miaka 50 ya madrasa hiyo, Naibu Mkuu wa KMKM, Kepteni Hussein Mohammed Seif, alikumbusha kuwa Mtume Muhammad hakuwa tu mfundishaji wa dini, bali pia alikuwa mtendaji wa matendo mema na mlezi wa jamii katika kila hali.


“Mtume hakutufundisha tu kwa maneno, bali kwa vitendo. Alifanya usafi, alisaidia masikini, aliwatembelea wagonjwa na alihimiza umoja. Haya ni mafundisho ambayo hatupaswi kuyasahau, hasa katika kipindi hiki tunapomkumbuka,” alisema Kepteni Hussein.

Aliwataka waumini kutambua kuwa usafi si amri ya kiafya pekee, bali ni sehemu ya imani, kwa kuwa Mtume alisema: "Uislamu ni usafi."


Aidha, Kepteni Hussein aliwataka viongozi na walimu wa madrasa nyingine kuiga mfano wa Swiffat Nabawiyatul-Kareem, akisema kuwa kushiriki shughuli kama hizo ni mchango mkubwa katika juhudi za serikali za kuimarisha ustawi wa jamii.


“Ni vyema tukajifunza kuwa na namna za kusherehekea Maulid zinazogusa jamii moja kwa moja kwa kuchangia damu, kufanya usafi, kutembelea wagonjwa, au kuwafariji wafiwa. Hii ndiyo njia bora ya kumuenzi Mtume Muhammad (S.A.W),” aliongeza kepteni Hussein.

Kwa Upande wake Naibu Amir wa madrasa hiyo, Rashid Abdallah Rashid, alisema kuwa lengo kuu la tukio hilo ni kuendeleza mapokeo ya Kiislamu yanayoleta jamii pamoja kwa kuonesha upendo, mshikamano, na maadili mema, hususan katika kushiriki shughuli za kijamii zinazolenga ustawi wa jamii

“Tunataka vijana wetu wajue kuwa Maulid si sherehe za kula na kuvaa tu, bali ni fursa ya kuenzi mwangaza wa Mtume na kuurithisha Kwa kizazi kijacho,” alisema Rashid.

Alieleza kuwa mbali na zoezi la usafi na uchangiaji damu, wameandaa  shughuli ya usiku wa zamani,  utakaopambwa na dufu la mitindo ya zamani na mavazi ya asili , ili kuwarithisha vijana wa leo utamaduni wetu wa Kiislamu,” alisema Rashid.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa madrasa hiyo, Abdalla Zubeir Marzuk, alisema katika wiki ya maadhimisho hayo wanatarajia kuwatembelea masheikh waasisi  waliolitumikia dini  na madrasa hiyo kwa miaka mingi, ili kuwafariji na kuwaombea dua waliotangulia mbele ya haki.

Alieleza kuwa suala la usafi si tu amri ya kidini bali pia ni agizo la kiafya linalpaswa kuendelezwa, kwani uchafu ni chanzo kikuu cha magonjwa mbalimbali katika jamii.

Katika tukio hilo, waumini, walimu na Wanafunzi walishiriki pia kupima afya na kuchangia damu wakitimiza kwa vitendo ile hadithi ya Mtume inayosema: “Mbora wenu ni yule mwenye manufaa kwa watu.”

Shughuli hiyo imeungwa mkono na vikosi vya KMKM, JKU, Zimamoto na makundi mbalimbali ya hamasa, wakitoa mchango wao kwa moyo wa heshima kwa Mtume wa mwisho na kipenzi cha Allah.