Popular services

WANAFUNZI WAHIMIZWA KUANZISHA KLABU ZA MAZINGIRA MASKULINI.

 NA FAUZIA MUSSA

WANAFUNZI wamehimizwa kuanzisha klabu za mazingira maskulini ili kushiriki katika utunzaji wa mazingira kwenye maeneo yanayowazunguka.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Mradi wa vijana wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, Khamis Ngwali Ali, alipokuwa akifugua mafunzo ya utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi wa skuli ya Tumekuja yaliofanyika Skulini hapo ikiwa ni sehemu ya utekelzaji wa mradi huo unaosimamiwa na jumuiya ya white star chini ya ufadhili wa Baraza la Jiji la Zanzibar.


“Tunahitaji kuona wanafunzi wakiongoza harakati hizi. Elimu mtakayopata leo isiishie hapa, bali ielekezwe kwenye vitendo, kuanzia skuli hadi majumbani kwenu,” alisema Ngwali.

Alisema klabu hizo zitakazokuwa chini ya usimamizi wa viongozi wa wanafunzi, walimu na walezi wa skuli, zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupanda na kuendeleza bustani ambazo zinaleta haiba nzuri katika maeneo mbalimbali.

Alisema bustani sio tu sehemu ya mapambo lakini pia sasa ni fursa ya bishara ambapo wengi wamefanikiwa kupitia upandaji wa bustani kupitia uzoefu walioupata katika klabu za mazingira maskulini.

“Tunataka kuona bustani za skuli zikihifadhiwa, zinatunzwa, na kuendelezwa. Bustani hizi hutoa hewa safi, hupunguza joto, na zinaweza hata kutoa ajira,” aliongeza Mwenyekiti huyo.


Mapema, alieleza kuwa White star inaandaa mikakati endelevu ya kuhakikisha kuwa juhudi hizo zinaendelea hata baada ya mradi kukamilika ikiwemo uendelezaji wa bustani, uanzishaji wa klabu za mazingira, na mafunzo endelevu kwa walimu na wanafunzi.

“White Star itaendelea kubeba ajenda hii kwa moyo wa kizalendo na uwajibikaji mkubwa kwa mustakabali wa mazingira yetu,  hatua hii inalenga kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha usafi wa miji na uhifadhi wa mazingira.” alieleza.

Alieleza kuwa mbali na elimu ya mazingira White Star ilianzisha bustani ya mfano katika skuli hiyo kupitia mradi huo, ikiwa ni hatua ya vitendo ya kuonesha njia sahihi ya uhifadhi wa mazingira kupitia elimu na ushirikiano. 

Kuhusu jumuiya ya white star alibainisha kuwa ilianzishwa mwaka 2002 na kusajiliwa rasmi kwa namba 202, ikilenga kuimarisha elimu, afya, mazingira, kilimo, lishe na uchumi wa buluu ambapo hadi sasa imefanikiwa kutekeleza zaidi ya miradi 30 ya uimarishaji wa ustawi wa jamii.


Akitoa mada katika mafunzo hayo ofisa kutoka Idara ya Mazingira, Zuwena Juma, aliwahimiza wanafunzi kushiriki  shughuli za upandaji miti, kuhamasisha wenzao na jamii juu ya masuala ya usafi, pamoja na kuwa na utamaduni wa kuweka taka kwenye maeneo rasmi kwa njia salama ili kuwa mfano wa kuigwa katika utunzaji mazingira.

Alifafanua kuwa mazingira ni muunganiko wa vitu vyote vinavyomzunguka binadamu, ikiwemo ardhi, mito, misitu, wanyama, hali ya hewa, na rasilimali nyingine za asili na kusisitiza kuwa kutunza mazingira si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja kwa nafasi yake.

“Mazingira ni uhai wetu. Tunapoyatunza, tunalinda maisha yetu, afya zetu, na ustawi wa vizazi vijavyo. Kupanda mti ni sadaka, na ni ibada kwa mujibu wa baadhi ya imani za kidini,” alisema Zuwena.

Aliwaeleza wanafunzi hao kuwa kuna aina kuu tatu za mazingira ambazo ni mazingira ya hewani, baharini, na ardhini ambapo kila moja inapaswa kuhifadhiwa kutokana na mchango wake mkubwa kwa ustawi wa maisha ya viumbe hai.


Alifahamisha kuwa endapo mazingira yatatunzwa yatasaidia kukuza afya za binaadamu na wanyama, kupunguza upotevu wa bioanuwai na upoteaji holela wa Maliasili za baharini na nchi kavu.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Tumekuja, Suleiman Salum Abdalla, aliishukuru Jumuiya ya White Star kwa kuchagua skuli hiyo kuwa sehemu ya mradi huo, na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi wa mazingira ndani na nje ya skuli.

“Tunaiona hii kama fursa ya kipekee kwa wanafunzi wetu. Kupitia elimu hii, tunawajengea misingi ya kuwa viongozi wa kesho katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Mwalimu Suleiman.

Nao Wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo walielezea kuridhika na Elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wa mazingira kwa jamii inayowazunguka. 

Miongoni mwa wanafunzi hao Muadhi Salmin Ali alisema atatumia elimu hiyo kuhamasisha jamii yake, huku Zamila Moh’d Ally akisisitiza kuwa jamii nzima inapaswa kuchukua hatua za uhifadhi wa mazingira kama sehemu ya maisha ya kila siku.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliwashirikisha wanafunzi 85 wa skuli ya Tumekuja ambao wanatarajiwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea na kuhifadhi mazingira ambayo ni urithi wa dunia na zawadi kwa vizazi vijavyo.