Katika jamii ya mkoa wa Kaskazini Unguja, wanawake bado wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kuingia kwenye nafasi za uongozi, Mitazamo potofu inayotokana na mila, silka na utamaduni wa Kizanzibari mara nyingi ni kikwazo kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi wa kijamii.
Hata hivyo, jitihada za serikali na taasisi mbalimbali zimeanza kubadilisha taswira hii kupitia mafunzo ya uongozi na programu za uhamasishaji. Mafunzo haya yanalenga kuwapa wanawake mwangaza wa kuona fursa zilizopo na kuzikimbilia, huku likilenga kufanikisha usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake katika nafasi za uongozi.
Fat-Hiya Pandu Juma, mkazi wa Shehia ya Kikobweni, Wilaya ya Kaskazini A, ni miongoni mwa wanawake waliyonufaika na mafunzo ya uongozi ambayo, yalimjengea kujiamini na kumpa uthubutu wa kuwania nafasi za kisiasa. Hatua yake ya kuchukua fomu ya kugombea Uwakilishi Jimbo la Mkwajuni kupitia chama cha ADA-TADEA anaiona kama mabadiliko makubwa baada ya kushiriki mafunzo ya wanawake na uongozi ndani na nje ya mkoa. Fat-Hiya anasema.“Kiukweli mafunzo ya wanawake na uongozi kutoka TAMWA-ZNZ, NAPAC na JUVIEKA yamenijengea uwezo mkubwa mpaka kufika hapa. hapo awali sikuwa na uthubutu huu.”
TAMWA-ZNZ, imekuwa mstari wa mbele katika kuinua uwezo wa wanawake wa Zanzibar kisiasa, kijamii na kupitia vyombo vya habari. Kupitia mradi wa Strengthening Women in Leadership (SWIL) na miradi mingine, zaidi ya wanawake 6,000 walipata mafunzo juu ya haki zao za kiraia na ushiriki katika maamuzi. Mamia ya wafanyakazi wa kijamii waliandaliwa kuwa watetezi wa haki za wanawake, huku waandishi wa habari na vijana wakijengewa uwezo wa kuandika na kuripoti habari zinazohamasisha usawa wa kijinsia. Zaidi ya wananchi 11,000 walihusishwa kwenye mikutano ya elimu ya uongozi na haki, huku wanawake 200 wakipata mafunzo maalum ya siasa, demokrasia na uongozi.
Asia Fadhil Makame,Mkurungezi wa Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A(NAPAC) ameeleza kuwa kupitia mradi wa Sauti ya Mwanamke uliofadhiliwa na European Union, zaidi ya watu 5,000 wakiwemo wanawake wamepata elimu ya kisheria na uongozi. “Kupitia mradi wa Sauti ya Mwanamke uliofadhiliwa na European Union kupitia ENABEL na LSF, zaidi ya watu 5,000 wengi wao ni wanawake tumewapa elimu kuhusu masuala ya kisheria na uongozi ili kufikia haki zao za kimsingi licha ya changamoto za kiuchumi,” alisema Asia. Mafunzo haya yamewasaidia wanawake kuzikimbilia fursa za uongozi na ajira katika mkoa huo.
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mkakati wa kuimarisha usawa wa kijinsia kupitia Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake 2023 na Mkakati wa Utekelezaji wa 2023–2033, unaolenga kuingiza jinsia katika bajeti, sera na mipango ya kitaifa. Zanzibar pia ilizindua rasmi Sera ya Jinsia kwa Vyama vya Siasa Disemba 2024, yenye lengo la kuhakikisha vyama vya siasa vina miundo thabiti ya kijinsia na kuongeza uwakilishi wa wanawake angalau asilimia 40. Idara ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake inahakikisha haki na usawa wa kijinsia kwa kuratibu masuala ya jinsia, kuingiza jinsia katika sera na mikakati ya serikali, na kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa. Kupitia mikataba kama CEDAW 1979, ICCPR 1966, Azimio la Beijing 1995, Itifaki ya Maputo 2003 na Mkataba wa SADC 2008, wanawake wanahimizwa kushiriki kwenye uchaguzi, kugombea nafasi za uongozi na kushiriki katika taasisi za serikali.
Licha ya mafanikio haya, changamoto bado zipo, Wanawake wengi wa vijijini hawajafikiwa na elimu ya uongozi, ukosefu wa rasilimali za kifedha unawakatisha tamaa, na mitazamo ya kijamii pamoja na mfumo dume katika siasa inaendelea kuwanyima nafasi sawa na wanaume.
Farihia Abdalla Juma, Katibu wa Jukwaa la Wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema: “Uwepo wa mafunzo ya uongozi umesaidia kuwainua wanawake Kaskazini Unguja kuzikimbilia fursa, lakini nguvu zaidi bado zinahitajika kufanikisha ushiriki wa wanawake katika nyanja zote za uongozi.”
Ili Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zifikie usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 katika uongozi, kunahitajika mshikamano mkubwa kati ya serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla. Mafanikio ya uthubutu wa Fat-Hiya na wanawake wengine ni dhahiri kuwa mabadiliko yanawezekana, ikizingatiwa kuwa sasa kuna haja ya kuimarisha utekelezaji wa sera, kuongeza rasilimali na kuondoa vizuizi vya kijamii.

