NA FAUZIA MUSSA
RAIS wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Asia Ramadhan Khamis, amewataka viongozi wapya wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kujitoa kwa dhati katika kuwasimamia na kuwatetea wanafunzi wanaowasimamia.
Akizungumza baada ya kuwaapisha Mawaziri na Manaibu Waziri wa Serikali hiyo, hafla iliyofanyika katika kampasi ya Tunguu, Asia alisema viongozi hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanaimarisha mahusiano kati ya walimu na wanafunzi kwa kuweka usawa, heshima, na nidhamu, ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi chuoni hapo.
Aidha alisema pia endapo Viongozi hao watasimamia majukumu Yao ipasavyo itasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi kitaaluma na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
“Sisi ndio sauti ya wanafunzi wa SUZA kwa mwaka wa masomo 2025 hadi 2026. Tunawajibu wa kuwatumikia wanafunzi kwa kuwawakilisha ipasavyo na kuwatetea pale inapobidi,” alisema Rais huyo wa SUZA.
Aliongeza kuwa SUZA ni taasisi ya elimu ya juu inayotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kupitia mafunzo yanayotolewa, hivyo ni muhimu kwa viongozi na wanafunzi wote kuwa na uadilifu, usikivu na nidhamu ili kufanikisha ndoto zao za kitaaluma na kijamii.
Aidha, Asia aliendelea kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na viongozi waliotangulia kwa juhudi zao katika kuweka mazingira bora ya kujifunzia SUZA, akisema kuwa mchango wao umeongeza ufanisi katika sekta ya elimu ya juu nchini.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi SUZA, Issa Harub Shaame, aliwahimiza viongozi walioteuliwa kutambua dhamana waliyopewa na kuhakikisha wanazingatia Katiba na Sheria za Serikali ya Wanafunzi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Naye Waziri Mkuu Mteule wa Serikali ya Wanafunzi, Yunus Farahani Mkanga, alitoa shukrani kwa viongozi wenzake kwa kumuamini na kumchagua kushika wadhifa huo na kuahidi kushirikiana nao kikamilifu katika kipindi chote cha uongozi wake.
“Umoja na mshikamano baina yetu ndio silaha ya mafanikio. Tukiwa kitu kimoja kati ya viongozi, walimu na wanafunzi, tutafanikiwa kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi na kuepuka changamoto zisizo za lazima,” alisisitiza Yunus.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chuo, watendaji wa idara, wanafunzi na wageni waalikwa ambapo viongozi hao waliapishwa rasmi kushika nyadhifa zao na kuanza rasmi majukumu ya uongozi wa Serikali ya Wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2025/2026.


