Popular services

MITANDAO YA KIJAMII: FURSA KWA WANAWAKE VIONGOZI KATIKA KUNADI SERA NA KUJITANGAZA


Nishan Khamis – Zanzibar.

Katika zama hizi za kidijitali, mitandao ya kijamii imekuwa chombo muhimu kwa viongozi na wanasiasa katika kujitangaza na kufikisha sera zao kwa wananchi. Kwa wanawake viongozi, ambao mara nyingi wamekumbana na changamoto za kijinsia na kijamii katika nafasi za uongozi, mitandao hii imefungua milango mipya ya fursa. Kupitia majukwaa kama Facebook, Instagram, TikTok na X, mwanamke anaweza kujijengea taswira yake, kuwasiliana moja kwa moja na wananchi na kushindana kwa usawa na viongozi wa kiume bila gharama kubwa za kampeni za kawaida.

Mitandao ya kijamii pia inawapa wanawake nafasi ya kuonesha uongozi wao kwa vitendo,matangazo ya moja kwa moja, mahojiano ya video na machapisho ya kila siku huwasaidia wananchi kuelewa msimamo wa kiongozi bila kupotoshwa na vyombo vya habari au wapinzani. Ni njia rahisi ya kunadi sera, kusikiliza wananchi na kujibu hoja mara moja. Hata katika jamii zinazomkandamiza mwanamke, mitandao imekuwa silaha ya kuvunja ukimya na kuthibitisha uwezo wake.

Hata hivyo, changamoto bado zipo. Uonevu wa kimtandao, mashambulizi ya maneno na taarifa za uongo hutokea zaidi kwa wanawake wanasiasa kuliko wanaume. Pia, pengo la teknolojia husababisha baadhi ya wanawake, hususan walioko vijijini, kutoweza kufikia mtandao au vifaa vya kidijitali.

Mfano halisi ni Rikizi Pemba Juma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar. Rikizi anatumia mitandao si tu kuhamasisha chama chake, bali pia katika majukumu yake ya uongozi na kukuza biashara zake binafsi. Anasema: “Mitandao ya kijamii ni fursa nzuri endapo itatumika vizuri, lakini pia ni sehemu hatarishi kwa udhalilishaji ikiwa haitatumika kwa uangalifu hivyo ni sehemu sahihi  ya kujitangaza kisera  na kiuongozi wanawake kwa kutambua ealimu sahihi ya mitandao kama fursa kwetu"

Kwa mujibu wa DataReportal na NapoleonCat, Tanzania ina watumiaji wa mtandao milioni 21.82 mwanzoni mwa mwaka 2024, ikihusisha asilimia 31.9 ya idadi ya watu wote nchini. Facebook ina watumiaji milioni 8.21, Instagram milioni 3.93, Messenger milioni 7.26, na LinkedIn milioni 1.50. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa mitandao ni nyenzo muhimu kwa mawasiliano na kujitangaza, lakini pia inahitaji uwajibikaji na elimu ya usalama mtandaoni.

Sheria na kanuni zinazosimamia mitandao nchini, ikiwemo Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya 2015, na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za 2020, zinabainisha wajibu wa watumiaji, kuzuia taarifa za uongo, lugha ya chuki na udhalilishaji. Pia zinahimiza maudhui yenye staha na kuheshimu maslahi ya umma, jambo linalofanya mitandao kuwa nyenzo yenye fursa, lakini yenye uwajibikaji.

Maryam Khamis, mgombea Uwakilishi Jimbo la Tumbatu kupitia chama cha UMD, amesema kuwa kwa sasa anatumia WhatsApp na TikTok kwa shughuli zake, lakini ana hamu ya kujifunza zaidi juu ya mitandao mingine ili kuiboresha harakati zake za kisiasa na kijamii"sina elimu ya kutosha juu ya matumizi ya mitandao kama fursa ila natumia tu kama kawaida ila natamani nijue ziadi ili nielimike na kutambua fursa zenyewe kwenye mitandao "amesema Maryam.

Selemani Makwita kutoka  Action for Democratic Governance anashauri wanawake viongozi kutambua lengo lao katika mitandao, kutumia akaunti rasmi na za kitaaluma, kulenga maudhui yenye thamani, kuepuka matusi, kutumia mbinu za usalama mtandaoni, kujifunza kuhusu ushiriki wa jamii, kutumia mitandao kwa matangazo rasmi, kufuatilia takwimu, na kupata msaada wa wataalamu. "Aidha, nasisitiza kufuata sheria, kanuni, na miongozo ya Mamlaka ya MawasilianoTanzania, taasisi kama Chama Cha Waandishi wa Habari WanawakeTanzania (TAMWA-ZANZIBAR) ,Chama cha wanasheria wanawake Zanzibar, Tume ya Utangazaji Zanzibar na mashirika mengine yanayohusiana na usalama mtandao masuala ya wanawake nchini "am3sema Makwita.

Nasra Nassor Omar, Naibu Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje kupitia ACT-WAZALENDO, amesema mitandao ni fursa muhimu kwa wanawake kuendeleza uongozi, shughuli za kiuchumi na kijamii, licha ya changamoto za unyanyasaji wa kimtandao." Kwa upande wa chama chetu tupo vizuri kwenye mitandao na tunahamasisha wanawake wajikite katika mitandao kwa kufuata taratibu na kanuni za matumizi ya mitandao kwa maslahi zaidi " Amesema Nasra.

Ripoti za Women at Web Tanzania (2022) zinaonyesha kuwa takriban asilimia 77 ya wanawake wanaojihusisha na siasa wamesimamisha kutumia mitandao kutokana na unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni, huku asilimia 73.1 wakiwa bila mafunzo ya kukabiliana na hali hiyo. Tafiti za 2024–2025 kutoka , Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Paradigm Initiative,Baraza la Habari kwa Maendeleo Tanzania na Jumuiya ya Vijana ya Uwezeshaji wa Kijinsia zinaonyesha wanawake viongozi kukumbana na unyanyasaji wa kimtandao mara 27 zaidi kuliko wanaume.

Dkt. Mzuri Issa, ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania -TAMWA-ZANZIBAR, amesema ukatili wa kimtandao ni miongoni mwa udhalilishaji ambao umekuwa ukiwazuia baadhi ya wanawake viongozi kushiriki kikamilifu katika siasa kwa kuhofia unyanyasaji."Watu washindane kwa hoja na sio kudhalilishana, huku suala la ushawishi la matumizi ya mitandao liwe suala mtambuka kwenye suala hili," Dkt. Mzuri amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii yatasaidia kuepusha wanawake na watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia mtandaoni na kuhakikisha mitandao haitumiwi kueneza vitendo viovu bali kuwa uwanja wa kukuza mijadala ya kuchochea maendeleo.