Na, Nishan Khamis – Shangani
Jumatatu, 22-2025.
Mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema atahakikisha anaongeza maslahi ya watumishi wa umma, kuendelea kuimarisha maendeleo katika nyanja zote zikiwemo za kijamii, kielimu, kimichezo, pamoja na kuwezesha mikopo isiyo na riba kwa maslahi ya maendeleo ya Wazanzibari.
Kauli hiyo ameitoa wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shangani, Jimbo la Kijini, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo amesema ataendeleza kasi yake ya maendeleo pamoja na kuongeza pensheni ya wastaafu na pensheni jamii, kujenga viwanja vya michezo vya kisasa kila mkoa na wilaya, kutoa ajira, na kujenga viwanda ili wananchi waweze kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Amesema kadri uchumi unavyoongezeka, ndivyo serikali itakavyoongeza posho, fedha za kufanyia kazi katika wizara, huku akibainisha kuwa kwa sasa asilimia 60 ya makusanyo ya mapato yanatumika kulipa mishahara ya watumishi.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi wa mkoa huo na Zanzibar kwa jumla kuendelea kushirikiana, kushikamana na kudumisha amani na utulivu nchini, sambamba na kuwaomba ifikapo Oktoba 29 wajitokeze kwa wingi katika zoezi la kupiga kura kwa kuichagua CCM na viongozi wake wote ili kuendeleza maendeleo nchini.
Kwa upande wao, wananchi waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa kwa maendeleo makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Dk. Mwinyi, wana kila sababu ya kumuunga mkono kwa kumpigia kura ifikapo Oktoba 29, ili aendelee kusukuma gurudumu la maendeleo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

