Na, Nishan Khamis – Mkwajuni
Jumamosi, 20 Septemba 2025
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Iddi Ali Ame, amewataka wanachama wa chama hicho Jimbo la Mkwajuni na mkoa kwa ujumla kuendeleza mshikamano na mshirikiano, huku akihimiza kuachana na tabia za makundi ndani ya chama na badala yake kujikita katika kuhakikisha ushindi wa kishindo unapatikana ifikapo Oktoba mwaka huu ili CCM iendelee kushika dola nchini.
Akizungumza katika Ofisi ya Jimbo la CCM Mkwajuni leo Jumamosi, Mwenyekiti huyo amewataka wanachama wote kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Husein Ali Mwinyi, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Mapokezi hayo yatafanyika katika mkutano wa hadhara utakaopigwa Jumatatu, 22 Septemba 2025, Uwanja wa Mpira Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A.
Aidha, Iddi Ali Ame amesisitiza kuwa chama kinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na Kanuni zake, hivyo yeyote atakayejaribu kukwamisha maendeleo ya chama au kusaliti atachukuliwa hatua kali za kichama. Amewataka viongozi wa jimbo kuhakikisha maandalizi ya mapokezi yanafanyika kwa weledi na mshirikiano mkubwa, akibainisha kuwa mshikamano, umoja na mshirikiano ndiyo silaha ya ushindi wa CCM.
Kwa upande wao, viongozi wa Jimbo la Mkwajuni wameeleza kufurahishwa na ujio wa Makamu Mwenyekiti wa CCM na kuahidi kuyatekeleza kwa vitendo maagizo yote yaliyotolewa.
Naye kwa upande wao wanachama walioshiriki kikao hicho wamemhakikishia Mwenyekiti huyo kuwa hawatamuangusha, na ifikapo siku ya kupiga kura wataelekeza kura za “NDIYO” kwa viongozi wote wa CCM katika jimbo na taifa kwa ujumla.
