Popular services

“UNDP, ZLSC Wawawezesha Wanawake Kupata Haki Zao Kisheria”

 “UNDP, ZLSC Wawawezesha Wanawake Kupata Haki Zao Kisheria”

NA FAUZIA MUSSA

MKURUGENZI wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Felista Mauya, ameeleza kuwa huduma za msaada wa kisheria bila malipo ni njia muhimu ya kuhakikisha haki inawafikia watu wote, hususan walioko vijijini na wenye kipato kidogo.


Akizungumza na wanawake wa vikundi vya ujasiriamali katika Shehia ya Kikungwi, Felista alisema wanawake na wasichana wengi hukumbana na changamoto za kisheria lakini hukosa uelewa na uwezo wa kuzitatua kupitia mfumo wa sheria. 

Alisisitiza kuwa kusogeza huduma hizo karibu na wananchi ni hatua muhimu ya kuwawezesha kupata haki zao kwa usawa na kwa wakati.

“Wananchi wengi hawawezi kumudu gharama za wanasheria au kwenda mahakamani. Kupitia huduma za msaada wa kisheria bila malipo, mtu anapata usaidizi wa kitaalamu bila kuhangaika na gharama kubwa. Hii inaongeza usawa na uwajibikaji katika jamii,” alisema Felista.


Aliongeza kuwa huduma hizi si tu kwamba zinaongeza uelewa wa sheria kwa wananchi, bali pia zinawapa ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika kutafuta haki zao na kushiriki kwenye utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani.

Felista alibainisha kuwa huduma hizo zinatoa ulinzi maalum kwa makundi ya watu wanaokabiliwa na changamoto zaidi kama wanawake, watu wenye ulemavu, wazee na wanaoishi maeneo ya vijijini.

“Makundi haya mara nyingi hayawezi kusikilizwa au kushiriki katika mfumo wa sheria kwa sababu ya ukosefu wa elimu ya sheria au uwezo wa kifedha. Msaada wa kisheria bila malipo unawapa sauti na fursa ya kusikilizwa,” alifafanua.


Aliwahimiza wanavikundi kuwa na katiba za vikundi vyao, kuzisoma na kuzitumia kama mwongozo wa haki na wajibu wa kila mwanachama na kuwahamasisha kutembelea ofisi za ZLSC pale wanapokumbana na changamoto za kisheria au wanapohitaji ushauri wa kitaalamu katika masuala ya sheria.

Mapema alieleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kujenga uwezo kwa wanawake kuelewa haki za msingi, sheria muhimu za maisha ya kila siku, na namna ya kushiriki katika kutetea haki na kushughulikia migogoro kwa njia ya amani.

“Lengo ni kuwafikia wananchi 4,000 wasio na uwezo wa kumudu gharama za wanasheria, wakiwemo wanawake, watoto, vijana, na watu wenye ulemavu katika wilaya zote za Unguja,” alisema Fiesta.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dk. Sikujua Omar Hamdan, aliwataka wanawake hao kutambua haki zao kisheria na kufuatilia masuala yanayohusu malezi ya watoto, urithi, na umiliki wa ardhi.

“Msaada wa kisheria unajumuisha huduma za ushauri, uwakilishi wa kisheria bila malipo au kwa gharama nafuu. Lengo ni kuhakikisha kila mtu anapata haki zake bila kujali hali yake ya kiuchumi,” alisema Dkt. Sikujua.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa ZLSC, Denis Joseph, aliwataka wanawake kutokaa kimya wanapokutana na changamoto za kisheria na badala yake wapaze sauti, wajue ni aina gani ya kesi wanaweza kufikisha na wapi pa kwenda kupata msaada.

 “Tunatarajia kuwa na jamii inayotambua haki zao na kutumia njia ya amani na sheria kutatua migogoro. Huduma ya msaada wa kisheria ni nyenzo muhimu ya kudumisha haki, usawa, na amani katika jamii,” alisema Denis.

Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imetoa mwanga kuhusu haki zao na umuhimu wa msaada wa kisheria katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Miongoni mwa washiriki hao, Msaidizi wa Sheria wa Wilaya ya Kati, ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Uvuvi Kikungwi, Bahati Issa Suleiman, alieleza kuwa wanapokea malalamiko mengi, lakini wanawake wengi bado hawako tayari kusaidiwa kisheria, wakipendelea kuyamaliza matatizo katika ngazi ya familia.

Katika huduma hizo zinazoendelea kutolewa na ZLSC kupitia programu ya msaada wa kisheria wa kuhamahama chini ya ufadhili wa mradi wa uwezeshaji kisheria unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), mada mbalimbali zinawasilishwa ikiwa ni pamoja na haki za Binadamu na Kikatiba, Sheria za Familia, Sheria za Ardhi na Makazi, sheria za kazi na ajira, sheria za makosa ya Jinai, pamoja na mbinu za kupata msaada wa kisheria.

Vikundi vilivyoshiriki katika mafunzo hayo ni pamoja na Kikundi cha Hata Wewe, Kikundi cha Nasie Roho na Kikundi cha Mwenye lake Aseme, abebwae hujikaza, chaza mali, mkorofi si mwenzetu  na ufisadi mbaya.