WATU WENYE ULEMAVU WAPATIWA MAFUNZO YA BIASHARA: TAMWA ZNZ, SHIJUWAZA NA ZANAB WAIMARISHA UWEZESHAJI KIUCHUMI KUSINI UNGUJA
NA FAUZIA MUSSA
Jumla ya wanachama 25 kutoka vikundi 16 vya kuweka na kukopa (SACCOS) Wilaya ya Kusini Unguja wamepatiwa mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kuchagua, kupanga na kusimamia biashara, chini ya Programu ya Mashirikiano ya Pamoja kwa ajili ya Haki za Watu wenye Ulemavu (CADiR).
Kati yao 16 ni watu wenye ulemavu na 9 ni walezi au wasimamizi wa watoto wenye ulemavu.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, yaliofanyika Ukumbi wa Walimu Kitogani, Mratibu wa Programu ya CADiR kutoka NAD, Aziza Ismail, alisema taasisi zinazotekeleza mpango huo zinaamini kuwa elimu hiyo italeta mabadiliko chanya kwa jamii ya watu wenye ulemavu.
“Kwa vile moja ya malengo makuu ya programu hii ni kuwainua kiuchumi watu wenye ulemavu na kuwawezesha kupata kipato rasmi, tunaamini mafunzo haya ni chachu ya mabadiliko ya kweli,” alisisitiza Aziza.
Kwa Upande wake mkufunzi kutoka TAMWA ZNZ, Muhidini Ramadhan, aliwahimiza washiriki kutumia maarifa waliyopewa kwa vitendo akisema kuwa umasikini miongoni mwa watu wenye ulemavu unaweza kupungua ikiwa wataelimishwa kuhusu miradi ya kiuchumi yenye tija.
Naye Nairat Ali, Meneja wa Programu kutoka TAMWA ZNZ, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha wanachama kupanga biashara zenye malengo endelevu na kujitegemea kiuchumi.
“Tunaamini kwa kuanza na mipango mizuri ya biashara, vikundi hivi vitaweza kujiendesha vyenyewe na kuleta maendeleo kwa wanachama wao,” alisema Nairat.
Wakati huo huo, Khamis Ali, ofisa Program kutoka ZANAB, aliwasihi washiriki kuwa makini na kutumia vyema elimu waliyoipata kwa kuchagua biashara sahihi zitakazowawezesha kupata mikopo na kuirejesha kwa wakati.
Katika hatua ya Mafunzo Kwa vitendo, washiriki walijadili na kuandika mipango ya biashara huku baadhi wakielezea ndoto zao za kukuza miradi ya kilimo, ufugaji, ushonaji na biashara ndogondogo.
Yusra Ali Hassan, Msaidizi Katibu wa kikundi cha Mtu ni Utu cha Kajengwa, alisema mafunzo hayo yamempa mwanga mpya kuhusu namna ya kupanga matumizi kwa busara na kukuza biashara.
“Kupitia mafunzo haya tumejifunza kupanga matumizi kwa uangalifu na kuweka mipango thabiti ya biashara. Nimepata maarifa mapya ya kuendeleza biashara yangu ya ushonaji,” alisema kwa furaha.
Washiriki hao waliahidi kupeleka elimu hiyo kwa wanachama wengine ili kila kikundi kinufaike na kuimarika kiuchumi.
"Kwa jitihada hizi, matumaini ni kwamba jamii ya watu wenye ulemavu itapata nafasi ya kuinuka kiuchumi, kujitegemea, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa." Walisema
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), kwa kushirikiana na Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) na Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB), kwa msaada wa Shirika la Watu Wenye Ulemavu la Norway (NAD) yamelenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kuimarisha vikundi vya kuweka na kukopa katika wilaya 11 za Unguja na Pemba.
