NA FAUZIA MUSSA
Mwanasheria wa kamati ya jinsia na ukimwi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Hamud Haji Machano, ameitaka Jumuiya ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (ZAPHA+) kuwatambua watoto walioko chini ya malezi yao kwa vipaji walivyonavyo ili kuwawezesha kusaidiwa kulingana na uwezo wao binafsi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo elekezi ya kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na homa ya ini 'B' kwa viongozi wa ZAA, yaliofanyika Maji house, Machano alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwagawa watoto hao kisekta, jambo litakalorahisisha utoaji wa misaada kwa mujibu wa mahitaji ya kila mmoja.
“Tunapowagawa kisekta, inakuwa rahisi kuwasaidia kulingana na taaluma yao,” alisema.
Machano alisisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yanahitaji mipango madhubuti, huku akitoa wito kwa Kamati ya UKIMWI na Jinsia ya ZAA kuendeleza mikakati yenye tija kwa taasisi na jamii kwa ujumla.
Aidha, alieleza kuwa ZAA itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya UKIMWI kwa kutoa msaada pale inapohitajika.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya UKIMWI na Jinsia ya ZAA, Hamida Ubwa Mamboya, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utaratibu wa kuwafikia wafanyakazi wote, na kwa kuanzia wameanza na viongozi wa kamati kabla ya kuwafikia wengine.
Naye Mratibu wa Kamati hiyo, Ahmed Rajab Mwinyi, alisema kuwa kamati imeanzisha darasa maalumu mara mbili kwa wiki kwa ajili ya kutoa elimu ya UKIMWI, homa ya ini na mafunzo ya ustadi wa maisha.
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo inawapatia wafanyakazi wanaoishi na VVU posho ya shilingi 500,000 kila mwezi, huku akiwahimiza wengine kujitokeza kunufaika na mpango huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya UKIMWI Zanzibar, Dk. Ahmed Moh’d Khatib, alisema maambukizi mapya na vifo vinavyotokana na UKIMWI vimepungua, huku akibainisha kuwa bado kuna changamoto ya unyanyapaa, ingawa hali hiyo imeanza kubadilika kutokana na juhudi za taasisi kama ZAPHA+.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZAPHA+, Seif Juma Abdalla, alisema jumuiya hiyo kwa sasa inalea watoto wapatao 3,000, wakiwemo wanaoishi na VVU na wale ambao wazazi wao wana virusi hivyo.
“Watoto hawa wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo matatizo ya kisaikolojia, hivyo tumeanzisha klabu za ushauri katika wilaya zote za Unguja na Pemba japokuwa tunakabiliwa na ukosefu wa fedha,” alisema.


