Popular services

ACT WAZALENDO WAANZA KAMPENI ZA UBUNGE MKWAJUNI, MGOMBEA AHIDI ZAWADI KWA WANAFUNZI NA MSAADA KWA WALIMU WA MADRASA


Nishan Khamis, Mkwajuni — Agosti 31, 2025

Kampeni za uchaguzi wa Ubunge zimeanza rasmi katika Jimbo la Mkwajuni, ambapo mgombea ubunge kupitia chama cha ACT Wazalendo, Shaaban Majid Haji, leo amefanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mnanisisni na kujinadi kwa wananchi kwa kueleza vipaumbele vyake endapo atachaguliwa kuwa mbunge.

Akizungumza katika mkutano huo, Shaaban Majid Haji ameahidi kuwekeza katika elimu kwa wanafunzi wa jimbo hilo, akibainisha kuwa kila mwanafunzi atakayefanya vizuri zaidi darasani atazawadiwa. Ameeleza kuwa zawadi hizo zitatolewa kuanzia mwanafunzi wa kwanza hadi wa tano katika kila skuli ya Jimbo la Mkwajuni.

Aidha, akigusia malezi ya kijamii na kidini, mgombea huyo ameahidi kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuwa mbunge, atawawezesha walimu wa madrasa kwa kuwasaidia kupata huduma ya maji ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na malezi ya watoto wa jimbo hilo.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo walipokea ahadi hizo kwa mitazamo tofauti; baadhi wakiashiria matumaini mapya kwa maendeleo ya watoto na vijana, huku wengine wakisisitiza kuwa ni muhimu kwa mgombea huyo kuzitekeleza ahadi hizo iwapo atachaguliwa.