Popular services

MIAKA 5 YA UDIWANI,FATMA MNGWALI KHAMIS AANDIKA HISTORIA KAMA MWANAMKE WA KWANZA MWENYE ULEMAVU KASKAZINI UNGUJA.


Nishan Khamis – Zanzibar

Katika medani ya siasa za Zanzibar, jina la Fatma Mngwali Khamis limeibuka kama alama ya uthubutu na uongozi jumuishi. Alichaguliwa mwaka 2020 kuwa Diwani wa CCM Wilaya ya Kaskazini A , nafasi ambayo ameigeuza kuwa jukwaa la kusimamia maendeleo yanayogusa kila mwananchi.

Akijulikana kwa kupigania usawa na fursa sawa kwa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana, Fatma ameweka msingi wa uongozi unaoamini katika mshikamano na huduma bora kwa jamii. Safari yake inathibitisha kwamba uongozi siyo hadhi ya mtu binafsi, bali ni wajibu wa kuondoa vikwazo na kufungua njia kwa wengine.

Fatma alizaliwa mwaka 1977 katika kijiji cha Fukuchani, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Safari yake ya elimu ilianza mwaka 1981 katika Skuli ya Uhuru Mchanganyiko jijini Dar es Salaam, kisha mwaka 1992 akaendelea na masomo ya sekondari huko Korogwe, Tanga. Mbali na majukumu ya kifamilia kama mama wa watoto wanane, mwaka 2006 alijikita katika ufugaji wa kuku, jambo lililomjengea misingi ya kiuchumi na kujitegemea.

Mwaka 2014, aliamua kuingia kwenye siasa kupitia CCM, akivutwa na hamasa ya kuwatetea watu wenye ulemavu. Akizungumzia safari yake, Fatma anasema: “Nilichagua kusimama imara kwa sababu nilijua natetea haki za watu, siyo maslahi binafsi. Nimejifunza kuwa ulemavu si kikwazo, bali ni nguvu ya kuthibitisha kwamba kila mtu ana nafasi ya kuongoza.”

Katika kipindi chake cha udiwani, Fatma amejipambanua kwa kusimama imara kwenye vikao vya maendeleo ya wilaya na kushirikiana na madiwani wenzake kusukuma miradi ya kijamii. Amefanikisha miradi kama uchimbaji wa kisima cha maji katika kijiji cha Mjimwema, Matewme pamoja na kushughulikia changamoto ya umeme katika kijiji cha Kijambani.

Safari yake haikuwa rahisi,amekumbana na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kazi vinavyohitajika kwa mtu mwenye ulemavu, pamoja na unyanyapaa kutoka kwa baadhi ya watu waliodhani hawezi kumudu nafasi ya uongozi. Lakini hakukata tamaa.

Mumewe, Faki Mshenga, amekuwa nguzo muhimu katika maisha na safari ya kisiasa ya Fatma. Akizungumzia mchango wa mke wake, Faki alisema“Mke wangu ni mwanamke shupavu,Kila wakati amesimama kwa ajili ya familia na jamii na  mimi nitabaki kumpa ushirikiano hadi atakapofanikisha malengo yake. Wito wangu ni wanaume wasimame bega kwa bega na wake zao wanapojitosa kwenye nafasi za uongozi.”

Kwa upande wake, Twalib Haji Abas, Naibu Meya wa Baraza la Manispaa Kaskazini A, anasema: “Katika vikao vya baraza, Fatma amekuwa akileta hoja zenye mashiko na mapendekezo bora zaidi. Amejitambulisha kama kiongozi asiyeogopa kutetea maslahi ya watu wenye ulemavu na makundi maalum. Ni mwanamke wa kuigwa katika wilaya yetu na mkoa kwa ujumla.”

Kwa ujasiri wake, Fatma anaendelea kusimama kama sauti ya matumaini kwa wanawake na watu wenye ulemavu. Amekuwa akisisitiza: “Kila mtu ana nafasi yake kwenye siasa na maendeleo ya nchi, tusikubali kunyanyapaliwa au kuonekana hatuna uwezo. Tukisimama pamoja, tunaweza kufanikisha mambo makubwa.”

Safari ya Fatma Mngwali Khamis inabaki kuwa ushuhuda kwamba mwanamke mwenye ulemavu anaweza kusimama na kuwa kiongozi thabiti – kiongozi wa jamii, familia na taifa.