Popular services

MCT Yawataka Waandishi Kujua Sheria Ili Kujilinda, Yaahidi Msaada wa Kisheria

 MCT Yawataka Waandishi Kujua Sheria Ili Kujilinda, Yaahidi Msaada wa Kisheria

NA FAUZIA MUSSA

Baraza la Habari Tanzania (MCT), limedhamiria kuimarisha ulinzi wa waandishi wa habari kwa kuhakikisha wanapata msaada wa kisheria, elimu ya maadili, na uelewa wa sheria zinazowaongoza. 

Akizungumza na waandishi hao wakati akifungua mafunzo yalioambatana na klinik ya msaada wa kisheria Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Ernest Sungura aliwahimiza kuchukua hatua za kujilinda kisheria kwa kutafuta ushauri, kuzingatia ukweli, na kuwa na maadili katika kazi zao.


Alieleza kuwa ni muhimu kwao  kuwa na uelewa wa sheria zinazoongoza taaluma yao ili kuepuka migongano ya kisheria ambayo inaweza kuathiri kazi zao au kuwapelekea matatizoni.

 “Mnapaswa kuzijua na kuzizingatia sheria za habari, kufuata maadili na taratibu za kazi. Hii itawasaidia kufanya kazi kwa weledi bila kuvunja sheria au kuhatarisha usalama wenu na kujilinda wakati wote mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku.” alisema Sungura.

Mapema aliwahimiza kuipokea na kutumia fursa ya msaada wa kisheria inayotolewa na MCT, akibainisha kuwa baraza hilo limeanzisha huduma hiyo kwa waandishi ili kuwawezesha kutatua changamoto wanazokumbana nazo katika kazi zao.


“Tumeanzisha kliniki ya kisheria katika ofisi zetu kwa lengo la kuwapatia waandishi sehemu ya kutegemea wanapokutana na changamoto za kisheria. Tunatambua kuwa wanakumbana na vitisho, kunyimwa taarifa na hata kushitakiwa, hivyo msaada huu ni muhimu sana kwao,” aliongeza Sungura

Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa MCT Ziada Kilobo alisema uzoefu unaonesha kuwa waandishi wanakupambana na madhila mara Kwa mara ikiwemo kunyimwa taarifa na kupelekea  hata umma unaowategemea kukosa taarifa hizo.

Alisema Kwa muda mrefu Wamekua wakikosa Msaada wa kisheria pale  wanapokumbana na changamoto hizo na kupendekeza kuanzishwa kwa madawati ya msaada wa kisheria katika vyombo vya habari ili kusaidia waandishi kupata ushauri wa kisheria wakati wote.

Alieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia pia kutafuta Msaada wa kisheria  kabla ya kuchapisha habari, hususan zile za uchunguzi.

Aidha aliwasisitiza kuhakikisha kuwa habari wanazotoa ni za kweli, sahihi na zinazozingatia maadili ya uandishi na kuwataka kuwashirikisha wanasheria kabla ya kuchapisha habari zinazoweza kuibua athari za kisheria.

"Waandishi wanapaswa kuhakikisha habari zao zina ukweli na ushahidi wa kutosha, hasa zile za uchunguzi. Ni muhimu pia kujua kuwa kila habari inaweza kuwa na athari kisheria, hivyo mashauriano na wanasheria ni muhimu," alisisitiza kilobo.

Akitoa mada kuhusu haki ya kupata taarifa, Wakili msomi Hassan Kornely Kijogoo, alisema haki hiyo ni ya msingi na imeanishwa wazi katika Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 18(1) na (2).

“Kila mtu ana haki ya kupata taarifa, kutoa maoni na kushiriki katika mchakato wa mawasiliano bila ya kuingiliwa. Hii ni haki ya kikatiba ambayo huchochea uwajibikaji na maendeleo ya taifa,” alisema.

Aliongeza kuwa teknolojia imeongeza wigo wa upatikanaji na usambazaji wa taarifa, jambo linalowafanya wananchi wengi kuwa kama waandishi wa habari kupitia mitandao ya kijamii. 

Hata hivyo, alisisitiza kuwa matumizi ya haki hiyo yanapaswa kuzingatia maadili, sheria na kutolenga kumchafua mtu na utu wake na Kueleza chuki 

Ofisa kutoka Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu wakili Shadida Omar,  aliwakumbusha waandishi kuwa wana haki ya kupata taarifa kutoka mamlaka za umma na kuzisambaza kwa mujibu wa sheria. 

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kulinda chanzo cha habari, kuheshimu maadili na kuepuka migongano ya kimaslahi.

"Mwandishi ana haki ya kulindwa, kusikilizwa, na kusaidiwa kisheria. Hii itasaidia kuimarisha uhuru wa habari na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa wakati,” ilieleza Shadida.

Nao waandishi walioshiriki Mafunzo hayo walieleza kuridhishwa na huduma hiyo na kuiomba MCT kuifanya kuwa endelevu.

Walisema mafunzo hayo yamewakumbusha  kuhusu haki zao za kisheria na wajibu wao chini ya sheria za Zanzibar na kimataifa pamoja na Kuwajengea uwezo katika kushughulikia changamoto za kisheria wanapotekeleza majukumu yao.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliwakutanisha waandishi wa habari na wataalamu wa sheria  na  kujadili masuala muhimu ya kisheria yanayowahusu pamoja na Kutoa ushauri wa kisheria binafsi (one-on-one legal clinics) kwa waandishi wanaokumbana na matatizo ya kisheria.