Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, amewataka wamiliki na waendesha magari ya kubebea mchanga pamoja na wachimbaji mchanga kufuata sheria za barabarani na taratibu zitakazowekwa za kuchimba mchanga katika maeneo maalum yatakayotengwa kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Akizungumza jana katika kikao kilichofanyika ofisini kwake Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, kikao hicho kiliwakutanisha wamiliki wa magari ya mchanga na wachimbaji mchanga kujadili mustakabali wa upatikanaji wa eneo maalum la kuchimba mchanga pamoja na utaratibu wa kisheria wa ulipaji wa vibali na usahihi wa magari yao. Aidha, imeelezwa kuwa mara taratibu zitakapokamilika, magari hayo hayataruhusiwa kusafirisha mchanga nje ya Mkoa huo.
RC Mattar alisema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira njema ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ya kuboresha mazingira ya wananchi kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Ndugu Joseph Kilange, alikemea vitendo vya baadhi ya magari ya mchanga kuvunja amani na sheria, akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu. Pia alibainisha kuwa wizara inaandaa mpango wa kisasa wa ulipaji vibali kwa njia ya mtandao na upimaji wa uzito wa magari, na kuwataka wadau kutoa ushirikiano katika utekelezaji wake.
Wadau wa mchanga waliohudhuria kikao hicho walimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa maamuzi ya pamoja na kuahidi kushirikiana kwa karibu, kutekeleza makubaliano, na kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa wenzao ili kudumisha mshikamano, amani na utulivu, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini.
Kikao hicho kimewakutanisha Wakuu wa Wilaya, vyombo vya ulinzi na usalama wa Mkoa, Wizara ya Maji, Nishati na Madini, wakurugenzi pamoja na wadau wa mchanga wa Mkoa huo.
