Jumatano, 24 Septemba 2025
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Iddi Ali Ame, amewataka wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi wa Kijiji cha Matemwe, Jimbo la Mkwajuni, kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi na kuachana na watu wasiokuwa na nia njema za kimaendeleo.
Amesema hayo leo katika uwanja wa mpira wa Tundagaa, Matemwe Kusini, Wilaya ya Kaskazini A, wakati wa mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wanachama na wananchi mbalimbali, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za CCM Jimbo la Mkwajuni.
Ameeleza kuwa chama hicho kimekuwa kikihimiza amani mara kwa mara kwa sababu maendeleo yanayofanywa na viongozi nchini yasingewezekana bila utulivu. Ameongeza kuwa wananchi hawapaswi kuuza utu wao kwa kupoteza tunu ya amani, bali washirikiane kuiendeleza.
Aidha, aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi tarehe 29 Oktoba, kuwachagua viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani, ili chama hicho kiendelee kuongoza na kusukuma maendeleo zaidi nchini.
Kwa upande wao, wagombea wa nafasi mbalimbali jimboni humo walisema kuwa kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025, chama kimefanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa zaidi ya asilimia 100, ikiwemo sekta za miundombinu ya barabara, elimu, afya, kilimo, michezo na uwezeshaji wa mikopo kwa wajasiriamali na wanafunzi wa vyuo. Walimpongeza Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa jitihada kubwa za maendeleo.
Wagombea hao walisisitiza kuwa endapo watapewa ridhaa tena, wataendeleza utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030 na kuwataka wananchi kuendelea kuilinda amani ya nchi.
Baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo walisema wameridhishwa na utekelezaji wa maendeleo katika jimbo lao, na wakaahidi kulipa fadhila kwa chama hicho kwa kura za ndiyo ifikapo tarehe 29 Oktoba. Pia waliomba mikopo kwa akinamama iendelee kuimarishwa ili kuwawezesha kiuchumi.


