Popular services

SERIKALI KUTUMIA SHILINGI BILIONI 58 KUJENGA BARABARA TATU KASKAZINI UNGUJA, MATEMWE KIJINI KUANZA RASMI.



Na,Nishan khamis KIJINI–MATEMWE,
Alhamisi Septemba 7, 2025

Waziri wa Ujenzi, Miundombinu na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed, amesema jumla ya shilingi bilioni 58 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa miradi mitatu ya barabara katika maeneo ya Mkwajuni–Matemwe, Mkwajuni–Kijini na Muyuni–Nungwi.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa miradi hiyo uliofanyika katika uwanja wa Skuli ya Msingi Kijini, Dk. Khalid alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 38 zitatumika kwa barabara ya Muyuni–Nungwi, huku shilingi bilioni 20 zikielekezwa katika ujenzi wa barabara za Mkwajuni–Kijini na Mkwajuni–Matemwe.

Alibainisha kuwa ujenzi huo utahusisha pia uwekaji wa taa za barabarani kwa lengo la kuboresha mandhari na kuimarisha usalama wa wananchi. Aliongeza kuwa barabara hizo zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili, isipokuwa barabara ya Muyuni–Nungwi ambayo inatarajiwa kukamilika baada ya miezi minne.

Dk. Khalid alisisitiza kuwa miradi hiyo inafadhiliwa na fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kulipa kodi kwa wakati ili kuunga mkono juhudi za maendeleo ya taifa. Aidha, alisema serikali inatarajia pia kujenga barabara katika vijiji vya Kigongoni, Kibeni na Mfurumatonga Juga Kuu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa ujenzi wa kilomita 277.7 Unguja na Pemba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Matari Zahoro Masoud, alisema miradi hiyo ni utekelezaji wa ahadi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye ameonyesha uongozi wa vitendo na uwezo wa kutimiza ahadi zake.

Alimhakikishia Waziri kuwa ofisi yake itashirikiana ipasavyo na wakandarasi hao, huku akiwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Mwinyi pamoja na kudumisha amani na utulivu, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Rashid Simai Msaraka, alisema ukamilikaji wa barabara hizo pamoja na ujenzi wa kisasa wa uwanja wa ndege wa Nungwi utakuwa chachu ya kufungua fursa za kiuchumi na ajira kwa wakazi wa wilaya hiyo. Alisema ushirikiano wa wananchi ni muhimu ili kuhakikisha miundombinu hiyo inaleta manufaa kwa wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.

Wananchi wa Kijini–Matemwe nao walieleza furaha yao kwa hatua ya serikali kuanzisha ujenzi huo, wakisema kwa zaidi ya miaka 75 wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya barabara mbovu. Waliahidi kushirikiana kwa karibu kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa mafanikio.