Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Ndugu Sufian Khamis Ramadhan, amesema Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 imekidhi vigezo na imegusa maisha ya kila mwananchi katika kuendeleza maendeleo ya nchi, kutokana na usimamizi bora wa viongozi wa chama hicho endapo wataendelea kupata ridhaa ya kushika dola.
MNEC Sufian aliyasema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi jimbo la Nungwi, uliofanyika katika uwanja wa mpira Fukuchani, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo alizungumza na wanachama wa CCM pamoja na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Amesema Ilani ya CCM imegusa kila sekta muhimu ya maisha ya wananchi, hivyo akawataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuwapigia kura viongozi wa CCM kuanzia marais wote wawili, wabunge, wawakilishi na madiwani, ili kuendeleza maendeleo endelevu ya jimbo, mkoa na taifa kwa ujumla.
Aidha, amesisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, huku akiwaonya kuepuka vishawishi vya watu wenye nia mbaya vinavyoweza kuhatarisha maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wao, wagombea wa nafasi mbalimbali katika jimbo hilo walisema endapo watachaguliwa watahakikisha wanasimamia ipasavyo changamoto zinazohusu elimu, afya, uchumi na masuala ya kijamii katika jimbo hilo.
Wamewataka wananchi kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazoendelea chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, hususan katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara, elimu na afya. Aidha, wameomba ifikapo Oktoba 29 wananchi wawapigie kura viongozi wote wa CCM nchini.
Nao baadhi ya wanachama na wananchi waliohudhuria mkutano huo walisema wanapongeza dira ya Ilani ya CCM ya miaka mitano ijayo, lakini wakaeleza bado kuna changamoto za upatikanaji wa maji, umeme na huduma za afya katika vituo vya jimbo hilo. Hata hivyo, waliahidi kuendelea kuiunga mkono CCM kwa kuhakikisha kura zote zinakwenda kwa wagombea wake na marais wote wawili ili kulipa fadhila za maendeleo yaliyopatikana.


