Ijumaa, 26-09-2025.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kaskazini A, Bi Lucy John Mpembo, leo ameendeleza harakati za kukitafutia ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukutana na makundi mbalimbali yakiwemo wajasiriamali wadogo, wawekezaji, waendesha bodaboda pamoja na wananchi katika Jimbo la Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na makundi hayo, Bi Lucy alisema utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025 umefanikiwa kwa kugusa kila nyanja za maisha ya wananchi ikiwemo afya, miundombinu ya barabara, elimu, uwezeshaji wa mikopo kwa wajasiriamali na wanafunzi wa vyuo vikuu, pamoja na ujenzi wa viwanja vya kisasa vya michezo. Alisisitiza kuwa wananchi wana kila sababu ya kuhakikisha ifikapo Oktoba 29 mwaka huu kura zote zinamwendea Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea Urais wa Tanzania, Dkt. Hussein Ali Mwinyi mgombea Urais wa Zanzibar, pamoja na wabunge, wawakilishi na madiwani wa CCM, ili chama hicho kiendelee kuongoza kwa maendeleo ya nchi.
Aidha, aliwahakikishia wananchi wa Nungwi kuwa tatizo la maji lipo katika mpango wa utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030, ambapo taratibu za uwekezaji wa tangi kubwa la maji zinaendelea, na akawataka wawe na subira wakati juhudi za kulitatua tatizo hilo zikifanyiwa kazi.
Vilevile, aliwaomba wananchi kuendeleza amani na utulivu, sambamba na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuwapigia kura wagombea wote wa CCM pamoja na kuiomba serikali kujenga soko kubwa la kitalii katika wilaya hiyo kutokana na kukua kwa utalii ndani ya hiyo ili kutengeneza ajira zaidi na kurahisisha upatikanaji wa huduma sehemu rais kwa watalii.
Kwa upande wao, wajasiriamali na waendesha bodaboda walitoa pongezi kwa uimarishaji wa miundombinu ya barabara katika jimbo hilo, huku wakiahidi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kuichagua CCM. Pia waliomba kuongezewa mikopo zaidi ili kujikwamua kiuchumi.

