Na Nishan Khamis – Mkwajuni
Mkwajuni, 03 Oktoba 2025 — Gari aina ya Private Hire lenye namba za usajili Z 641 PK limeacha barabara na kugonga nyumba katika eneo la Mkarafuu Pakacha, Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja majira ya saa 11:50 alfajiri.
Gari hilo lililokuwa likitoka mjini kuelekea Shamba Nungwi, liliendeshwa na Yussuf Juma Khamis (32), mkazi wa Mbuzini. Kwa mujibu wa mashuhuda, gari hilo liliigonga nyumba ya Mtumwa Khamis Haji, mkazi wa Shehia ya Mkwajuni, na kusababisha uharibifu katika baadhi ya sehemu za nyumba hiyo, hususan eneo la biashara lililopo ndani ya nyumba. Hata hivyo, hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha.
Akizungumzia tukio hilo, Sheha wa Shehia ya Mkwajuni, Jumbe Idi Jumbe, amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, na ametoa wito kwa madereva kufuata kanuni na sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuleta madhara kwa maisha na mali za wananchi.
