NA FAUZIA MUSSA
MAKAMU Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji Aziza Iddi Suwedi, amewasihi wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa kuhakikisha kuwa wanatoa nafasi kwa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi, kwa kuendesha kampeni jumuishi zinazoendana na mahitaji yao.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku moja kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka majimbo mbalimbali pamoja na wanawake wa viti maalum, Jaji Aziza alivitaka vyama vya siasa kuhakikisha kampeni zao ni jumuishi, hasa kwa kuwajali watu wenye ulemavu.
Alisema uzoefu unaonesha kuwa kundi la watu wenye ulemavu limekuwa likikosa fursa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi, hususan katika hatua ya kampeni na kuwataka kuchukua hatua thabiti za kuhakikisha kundi hilo haliachwi nyuma.
Aidha aligusia changamoto wanazokutananazo kundi hilo hasa katika kampeni, kuwa ni pamoja na kutotengewa maeneo maalum na ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.
“Kundi hili muhimu limekuwa likilalamikia kukosa ladha ya kampeni, hasa kwa watu wenye ulemavu wa kusikia, kutokana na kutokuwepo wakalimani wa lugha ya alama katika mikutano ya kampeni,” alisema Jaji Aziza.
Aliongeza kuwa mazingira yasiyo rafiki katika maeneo ya kampeni pia yamekuwa kikwazo kwa watu wenye ulemavu kuhudhuria mikutano na kusikiliza sera za wagombea, jambo linalozorotesha ushiriki wao katika mchakato wa kidemokrasia.
Kwa mujibu wa Jaji Aziza, wagombea wanapaswa kuandaa maeneo ya kampeni yanayofikika kwa urahisi na kuweka sehemu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ili nao waweze kupata fursa ya kusikiliza sera na maelezo ya wagombea.
Katika kuhakikisha kampeni zinakuwa jumuishi, alisisitiza umuhimu wa uwepo wa wakalimani wa lugha ya alama katika mikutano yote ya kampeni, ili watu wenye ulemavu wa kusikia waweze kupata taarifa sahihi kama wengine.
Mapema alitoa wito kwa wagombea kuendeleza amani, ushirikiano, na kutumia taaluma waliyoipata katika katika kuendesha shughuli za Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Wagombea waliopata mafunzo hayo waliipongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kutoa elimu hiyo na kuahidi kufuata maagizo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha kampeni zinakuwa si tu za amani na utulivu, bali pia shirikishi kwa makundi yote, wakiwemo watu wenye ulemavu.


