Popular services

WAGOMBEA WASISITIZWA KAMPENI ZA UJUMUISHI KUZINGATIA MAHITAJI YA WATU WENYE ULEMAVU.

 NA FAUZIA MUSSA 

WAKATI kampeni za vyama vya siasa zikiendelea maeneo mbalimbali visiwani zanzibar bado wagombea wanasisitizwa kuzifanya jumuishi kwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Wakizungumza na mwaandishi wa habari hii Baadhi ya watu wenye ulemavu waliaeeleza kuwa ushiriki wao bado ni mdogo katika kampeni zilizoanza kufanyika kutokana na kutokuwepo matayarisho ya moja kwa moja yanayozingatia mahitaji yao.


" Sisi watu wenye ulemavu tupo katika hatari nyingi  licha ya kuwa amani inasisitizwa kila ucho na inaendelea kuwepo lakini kwenye wengi kuna mengi ule wingi na mchangonyiko wa watu tofauti kwetu sisi ni kikwazo hivyo tunaomba  kuwekewa  eneo letu maalum ambapo hata wakati wa kumalizika mkutano na kuruhusiwa kuondoka tuzingatiwe  usalama wetu dhidi ya msongomano wa washiriki." walieleza 

Katika kuhakikisha ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye kupata sera za wagombea unafikiwa walivishauri vyama vya siasa kutenga bajeti maalum kwa ajili ya usafiri, shamiana na gharama za wakalimani ili kuwatafsiria sera za wagombea kama yanavyowekewa bajeti masuala mengine yakiwemo ya mapambo na burudani.

 “vyenginevyo suala la ujunuishwaji litabaki kuwa  maneno na kuishia maandishi  vitabuni. waliongeza

Jamila Borafya mwenye ulemavu wa uoni alisema yeye binafsi hadi sasa hajashiriki kampeni yeyote kutokana na hofu ya usalama wake na kuona ni bora  kufuatilia matukio hayo katika vyombo vya habari.

Hata hivyo alieleza kuwa vyombo vya habari navyo vinawaacha nyuma wenye ulemavu wa aina nyengine kama ya kutosikia kutokana na kukosekana wakalimani wa lugha ya alama na wengine wako nyuma na vyombo vya habari kutokana na hali zao za kimaisha.

“Ningeshauri kila chama kiwe na mkalimani wake kwa mfano kampeni za 2020  jimbo la kiembe samaki tuliwekewa shamiana maalum kwa ajili yetu na tulishiriki bila kikwazo chochote, hali kama hiyo tunaitarajia kwa majimbo yote kwenye kampeni za mwaka huu”. Alisema jamila

Akizungumza katika kipindi maalum kilichorushwa na shirika la utangazaji Zanzibar Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu Salma Saadat aliwahimiza wagombea kuweka mazingira rafiki kwa kundi hilo kushiriki na kusikiliza sera zao.

Akielezea tathmini ya ushiriki wao kupitia uzinduzi wa kampeni za kitaifa zilizofanyika siku za karibuni alisema kundi hilo limejitokeza lakini bado maombi yao hayajafanyiwa kazi na hivyo kuendelea kuwaomba wagombea kuanza kwa vitendo kufanya kampeni jumuishi.

Aliwaomba kuweka wakalimani kuwasaidia wenye ulemavu wa kusikia na kuweka eneo maalum ambalo si tu litawasaidia watu wenye ulemavu lakini pia watalitumia wazee na wanawake wajawazito.

Aidha aliwakumbusha kuwa kundi la watu wenye ulemavu nao ni wapiga kura halali na bila kupata sera watashindwa kumchagua kiongozi alie sahihi.

"Kama mnataka kura zetu lazima sera zenu zitufukie bila kujua muelekeo wenu tutashindwa kuwachagua" alisema Salma

Sambamba na hayo aliwahimiza kutotumia lugha za uchochezi na kuhubiri amani kwani uwepo wa utulivu katika mikusanyiko hiyo ni njia moja ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kushiriki.

"Uchaguzi ni mchakato wa mpito kuna maisha kabla, wakati na baada ya uchaguzi ni lazima amani na utulivu viendelee kutawala katika maisha yote yanayoendelea." Alisisitiza Salma

Kwa Upande wake Naibu Mkurungezi wa upelelezi na makosa ya jinai DCI Zuberi Chembela alisema jeshi la polisi litaendelea kulinda raia na wagombea wakati wote wa kampeni na lipo tayari kutoa kipao mbele kwa watu wenye ulemavu ili nao wasiachwe nyuma kwenye mchakato wa demokrasia.

Alieleza kuwa endapo wadau wa uchaguzi watazingatia sheria kanuni na taratibu zilizowekwa amani itaendelea kuwepo muda wote.

Aidha DCI Zuberi aliwaomba viongozi wa watu wenye ulemavu kushirikiana na jeshi la polisi kuona namna ya kulisaidia kundi hilo na kueleza kuwa jeshi la polisi litaanda warsha na kundi hilo kuwashajihisha kushiriki mikutano ya kampeni na kupiga kura ili kupata haki yao ya msingi ya kuchagua kiongozi anaewafaa.

Jumla ya watu wenye ulemavu aina tofauti 8021 wamejiandikisha kuwa wapiga kura  zanzibar wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi  (albino) 102, wenye ulemavu wa uoni 678,  wenye ulemavu wa kusikia 1607, ulemavu wa viungo 2048, ulemavu mwengine 1260 na  ulemavu wa macho 2326.