Jamii ya kijiji cha Kibuyuni inakabiliwa na changamoto kubwa ya utoro wa wanafunzi na ukosefu wa nidhamu kwa watoto walioacha skuli, hali inayohatarisha usalama na maendeleo ya elimu katika eneo hilo.
Hayo ameyasema Mwalimu msaidizi wa Skuli ya Msingi Kibuyuni, Musa Machano Mjomba wakati akizungumza katika ufunguzi wa programu ya usalama kwanza uliowakutanisha wazazi wa wanafunzi na jeshi la polisi mkoa wa kaskazini Unguja kikoa kilicho fanyika katika skuli ya kibuyuni wilaya ya kaskazini A Unguja, alisema baadhi ya watoto waliotoroka skuli wamekuwa wakirudi maeneo ya skuli na kufanya vitendo hatarishi kama kurusha mawe madarasani na kuwasha moto, jambo linalosababisha taharuki kwa walimu na wanafunzi walioko darasani. Aidha, alibainisha kuwa ushirikiano mdogo wa wazazi katika kukabiliana na tatizo la utoro unasababisha watoto wengi kujihusisha na tabia zisizofaa mitaani na skulini.
Kijiji cha Kibuyuni pamoja na vijiji jirani vya Gunda na Machepu vimetajwa kuwa maeneo yenye uhitaji mkubwa wa wazazi kukaa pamoja na kutathmini mwenendo wa malezi kwa watoto wao, ili kulinda maslahi ya familia na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Sajent Thabit Makame Haji kutoka Makao Makuu ya Polisi Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja, alisema programu ya Usalama Kwanza ni endelevu na inalenga kuwarejesha watoto shuleni, kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na kuimarisha usalama wa wanafunzi. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi na walimu katika kufanikisha malengo hayo.
Naye, Ali Machano Ali, mjumbe wa shehia akizungumza kwa niaba ya sheha, alikiri kuwepo kwa changamoto hizo miongoni mwa vijana wa shehia hiyo. Alibainisha kuwa miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuanzisha kamati maalum ya kushughulikia matatizo ya utoro na nidhamu, ili kujenga Kibuyuni yenye kizazi chenye maadili na elimu bora.
Wazazi walioshiriki mkutano huo nao walieleza kuwa ukosefu wa mshirikiano katika malezi, hususan wazazi wa kiume kukimbia majukumu yao na kuwaachia wanawake pekee mzigo wa malezi, ni moja ya sababu zinazochochea watoto kuacha skuli na kujiingiza katika makundi mabaya. Walisema hali hiyo inawaathiri watoto kimaisha na kielimu, hivyo wakaomba hatua zichukuliwe kwa haraka kudhibiti tatizo hilo

