Jumanne,10-09-2025.
Jumuiya ya Vijana na Elimu Kaskazini A (JUVIEKA) kwa kushirikiana na ActionAid pamoja na Global Platforms Tanzania, imeendelea na mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi chipukizi wa vijana katika nafasi za uongozi kisiasa na nyanja mbalimbali za maendeleo.
Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A, Mkokotoni, yakihusisha jumla ya washiriki 30 kutoka vyama vya siasa na taasisi za vijana.
Mkurugenzi wa JUVIEKA, Mbarouk Maalum Mohammed, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuandaa kizazi cha viongozi wenye maono mapya kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kisiasa.
Alibainisha kuwa taasisi itaendelea kutoa nafasi kwa vijana kupata elimu ya uongozi, ili kujenga jamii yenye viongozi wachapakazi, waadilifu na wenye kujali maslahi ya wananchi. Aidha, aliwasisitiza washiriki hao kuwa mabalozi wa amani na utulivu katika harakati zote za uchaguzi na akawahimiza kuzingatia mafunzo hayo ili kuleta mabadiliko ya maendeleo ya vijana nchini.
Kwa upande wake, Seleman Makwita kutoka Action for Democratic Governance (A4DG), Dar es Salaam, aliwasilisha mada mbalimbali ikiwemo ushiriki wa vijana katika siasa, mchakato wa uchaguzi, utawala bora na ajenda ya vijana Tanzania.
Makwita pia aliwanasihi waliokuwa kwenye mafunzo kwamba endapo watapata ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi, basi watoe kipaumbele katika kupambania maslahi ya vijana nchini, kwani kundi hilo ndilo nguzo ya maendeleo ya taifa.
Aidha, katika mafunzo hayo washiriki walipitia nyaraka muhimu zikiwemo Sera ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar 2023, Ilani ya Vijana Tanzania, Muongozo wa Bajeti Zanzibar, pamoja na majukumu ya viongozi wa mitaa ikiwemo diwani na sheha.
Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mafunzo, washiriki waliishukuru JUVIEKA, ActionAid na Global Platforms Tanzania kwa hatua hiyo. Walibainisha kuwa elimu waliyoipata imekuwa chachu ya kuwaandaa kwa nafasi za uongozi na wakaahidi kuyatendea kazi watakapopata ridhaa ya wananchi katika nafasi zao za uongozi.
Waliongeza kuwa wako tayari kuhamasisha vijana kushiriki kwa amani katika uchaguzi ujao, kutetea maslahi ya jamii, kutumia ipasavyo mitandao ya kijamii na kuendeleza mijadala kuhusu haki za mabadiliko ya tabianchi pamoja na afya ya akili kwa vijana.
