Popular services

AFISA ELIMU AWATAKA MASHEHA NA KAMATI ZA SKULI KUHAMASISHA UANDIKISHAJI WA WATOTO SKULI, WENYE ULEMAVU WASIFICHWE.

 

Na Nishan Khamis,
Mkwajuni
Ijumaa, 2 Januari 2026
Masheha na Kamati za Skuli Wilaya ya Kaskazini A wametakiwa kushirikiana ipasavyo katika kuelimisha jamii kuhusu uandikishaji wa watoto pamoja na kuunga mkono juhudi za maendeleo ya elimu zinazofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika wilaya hiyo.

Wito huo umetolewa leo na Afisa Elimu wa Wilaya ya Kaskazini A, Juma Mwadin Abdalla, wakati akizungumza katika kikao cha Masheha na Kamati za Skuli kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za wilaya hiyo, Mkwajuni. Kikao hicho kililenga kuhamasisha uandikishaji wa watoto pamoja na kuimarisha ushirikiano wa jamii katika kusimamia maendeleo ya elimu bora katika skuli za wilaya hiyo.

Amesema sera ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar haitaki kuona mtoto yeyote akibaki nyumbani endapo amekidhi vigezo vya kuandikishwa skuli. Aidha, amewasisitiza wazazi kuwaandikisha watoto wenye ulemavu, akibainisha kuwa nao wana haki ya msingi ya kupata elimu sawa na watoto wengine.

Afisa Elimu  ameeleza kuwa kuna mabadiliko ya mitaala ya elimu, hivyo jamii ina wajibu wa kuyapokea mabadiliko hayo na kushirikiana kikamilifu katika kuyasimamia. Amesisitiza umuhimu wa Masheha na Kamati za Skuli kuwa walinzi wa maeneo ya skuli na kuyatunza, akieleza kuwa kumekuwepo na matukio ya uvamizi wa maeneo ya skuli katika wilaya hiyo, hali inayoweza kukwamisha maendeleo ya elimu.

Halikadhalika, amesema wilaya hiyo ipo katika kipindi cha shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, huku ikiwa na miradi miwili ya kielimu. Hivyo, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika ufunguzi wa miradi hiyo na kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa mageuzi makubwa ya maendeleo ya elimu
yanayoendelea kutekelezwa wilayanihumo.

Wakitoa michango yao katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe wamesema bado kuna changamoto ya uvamizi wa maeneo ya skuli pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu uandikishaji wa watoto, hususan watoto wenye ulemavu. Wamesisitiza kuwa juhudi zaidi zinahitajika katika kuelimisha jamii ili kufanikisha maendeleo endelevu ya elimu kwa watoto wa Wilaya ya Kaskazini A.
Aidha, wameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na kupongeza juhudi za Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuiletea wilaya hiyo maendeleo, hususan ujenzi wa skuli zenye hadhi ya kisasa na mazingira bora ya kujifunzia kwa watoto.