Na,Nishan khamis, Nungwi.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya za uhakika na kuondoa changamoto ya wananchi kufuata huduma hizo katika maeneo ya mbali.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Nungwi, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Mheshimiwa Rahma Kassim Ali, amesema hatua hiyo ni ushahidi wa wazi wa matunda ya Mapinduzi na utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa uhakika kwa wananchi wote.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta ya afya ili kuwasogezea wananchi huduma karibu na maeneo yao ya makazi, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto ya umbali mrefu na gharama za kufuata matibabu.
Aidha, Mheshimiwa Rahma Kassim ameitaka Wizara ya Afya kuhakikisha kituo hicho kitakapokamilika kinakuwa na watumishi wa kutosha wenye sifa na uwezo wa kutoa huduma bora, sambamba na kuwepo kwa huduma ya ambulensi kwa ajili ya wagonjwa wa dharura.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, amesema Wizara ya Afya Zanzibar imejenga jumla ya vituo vya afya 142, ambavyo vimezingatia uwepo wa watoa huduma wenye elimu na viwango vinavyokidhi mahitaji ya utoaji wa huduma za afya.
Ameeleza kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya Nungwi uliwahi kusimama kutokana na changamoto ya eneo, hali iliyosababisha kuahirishwa kwa mchoro wa awali wa jengo na kuchelewesha kukamilika kwa ujenzi huo.
Amesema kituo hicho cha afya chenye ghorofa mbili kinatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 3.5 na kitahudumia zaidi ya wagonjwa 38,000, kwa kutoa huduma masaa 24. Ameongeza kuwa ujenzi ulianza Agosti 2024 na unatarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A”, Rashid Simai Msaraka, amesema mkoa huo umeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ya kijamii, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya vinavyoendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia iliyopo, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha ametoa pongezi za dhati kwa Rais Dkt Husein Ali Mwinyi na Dkt Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi mzuri wa kimaendeleo katika mkoa huo na taifa kwa ujumla ,huku akimuahkishia mgeni rasmi kuwa mkoa huo upo salama na wataendelea kuimarisha ulinzi na usalama zaidi kwa mashirikiano makubwa kwa wananchi.
