Popular services

BARAZA LA MANISPAA KASKAZINI A LATOA ELIMU YA KISHERIA KWA WAJASIRIAMALI KINYASINI, LASISITIZA USAFI NA UZINGATIAJI WA SHERIA

 

Na Nishan Khamis, Kinyasini
Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wilaya ya Kaskazini A wametakiwa kufuata sheria na kanuni za Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A katika utekelezaji wa shughuli zao za kibiashara, sambamba na kuzingatia suala la usafi wa mazingira kwa maslahi mapana ya kiafya kwa jamii katika maeneo yao ya biashara.

Wito huo umetolewa leo na Afisa Afya wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A, Sanani Said Ali, wakati akizungumza na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Soko la Kinyasini katika kikao maalum cha utoaji wa elimu ya kisheria kwa jamii kuhusu miongozo ya serikali za mitaa, ikiwemo vibali vya ujenzi, usafi wa mazingira pamoja na leseni za biashara.

Amesema kuwa sheria namba saba ya baraza hilo inamtaka kila mfanyabiashara kuwa na chombo maalum cha kuhifadhia taka pamoja na kuzingatia miongozo mbalimbali ya kiafya katika utekelezaji wa shughuli zao, ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko na uambukizaji wa maradhi mbalimbali. Ameongeza kuwa sheria hiyo pia inawataka mama lishe na baba lishe kuwa na vyeti vya afya kabla ya kuanza au kuendelea na shughuli zao za kibiashara.

Kwa upande wake, Afisa Uchumi na Wajasiriamali wa baraza hilo, Foum Haji Khatib, amewataka wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo wadogo pamoja na jamii kwa ujumla kufuata taratibu na miongozo sahihi juu ya upatikanaji wa mikopo ya asilimia 4, 4 na 2 inayotolewa kwa makundi maalum ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika wilaya hiyo.

Amesema baraza hilo limetenga fedha maalum katika makusanyo yake kwa ajili ya mikopo ya makundi hayo matatu ikiwa ni jitihada za serikali katika kuwawezesha na kuinua uchumi wa wananchi. Hata hivyo, amesema baadhi ya wananchi hushindwa kunufaika na mikopo hiyo kutokana na kutofuata taratibu na miongozo iliyowekwa, hivyo amewashauri kuzingatia masharti hayo ili kufanikisha maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Naye Diwani wa Wadi ya Kinyasini, Haji Kidawa Mkali, amewahimiza wananchi wa wadi hiyo kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo na kuwahakikishia kuwa atasimamia kwa karibu kuhakikisha wenye nia ya dhati wanapata mikopo hiyo. Aidha, amewasisitiza wananchi kuzingatia suala la usafi wa mazingira pamoja na kufuata sheria na kanuni zilizowekwa katika shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wao, wajasiriamali na wafanyabiashara waliohudhuria kikao hicho wameeleza kushukuru kwa elimu waliyoipata na kuahidi kuzingatia na kutekeleza maelekezo yote waliyopewa. Pia wameomba kuwepo kwa masharti mepesi zaidi katika upatikanaji wa mikopo hiyo ili kuwasaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi kwa maslahi yao binafsi na taifa kwa ujumla.