Popular services

MSTAHIKI MEYA AFUNGA MASHINDANO YA MPIRA WA WAVU MAPINDUZI CUP 2026, ASISITIZA AMANI, UTULIVU NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA.

 

Na Nishan Khamis, Matemwe
Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Kaskazini A, Mhe. Nyange Kher Ali, leo amekuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufungaji wa mashindano ya Mpira wa Wavu wa Ufukweni Mapinduzi Cup 2026, yaliyofikia tamati yake kwa mchezo wa fainali kati ya Weusi Alligator Chuo cha Mafunzo na Panther Palumbo Hotel Kaskazini.

Mchezo huo wa fainali umechezwa katika uwanja wa Malumbo Hotel – Mnemba View, uliopo Matemwe, Wadi ya Gamba, Jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, na umehudhuriwa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa michezo.
Katika mchezo huo, timu  Alligator Chuo cha Mafunzo imeibuka mshindi baada ya kuifunga Panther Palumbo Hotel kwa seti 2 kwa 1, na hivyo kujinyakulia medali pamoja na zawadi ya fedha taslimu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Meya Nyange Kher Ali amewahimiza vijana kuendelea kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali, akieleza kuwa michezo ni fursa muhimu ya kujikwamua kiuchumi na pia njia ya kuitangaza nchi kimataifa kupitia sekta ya michezo.

Ameeleza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa michezo katika maendeleo ya taifa, na chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, inaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo nchini ili kutoa fursa kwa vijana kuonesha vipaji vyao na kupunguza changamoto za ajira.

Aidha, Mhe. Meya amewasisitiza wananchi kuendelea kudumisha amani, upendo na utulivu, sambamba na kutunza usafi na mazingira, akibainisha kuwa Wilaya ya Kaskazini A na Zanzibar kwa ujumla ni kivutio kikubwa cha watalii, hivyo utunzaji wa mazingira ni njia muhimu ya kuvutia watalii na kuongeza pato la taifa,Kwa mujibu wa waandaaji, jumla ya timu 16 zilishiriki katika mashindano hayo ya Mpinduzi Cup 2026.