Popular services

MWAKILISHI VITI MAALUM MKOA WA KUSINI PEMBA, MARYAM SAID KHAMIS, AFIKA KISIWA PANZA KUSIKILIZA CHANGAMOTO ZA WANANCHI; AAHIDI KUSHUGHULIKIA TATIZO LA VYOO.

 

Na Nishan Khamis, Kisiwa Panza
Katika kuendelea na jitihada za kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Mhe. Maryam Said Khamis, amefanya ziara katika Kisiwa Panza kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi kwa maslahi ya maendeleo ya jamii.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Maryam amesema kuwa lengo la kufika kisiwani hapo ni kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi na wananchi, pamoja na kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi huku akiwahakikishia ndani ya miezi miwili anatakeleza ahadi yake katika kisiwa hicho.

Ameahidi kushirikiana na wananchi na viongozi wa ngazi zote katika kutafuta suluhisho la changamoto zao, huku akibainisha kuwa atazishughulikia changamoto hizo hususan zile za kijamii, ikiwemo tatizo la vyoo, ili kuhakikisha wananchi wa Kisiwa Panza wanapata maendeleo bora kama maeneo mengine nchini.

Nae,diwani wa wadi ya Kangani Abdalla Khafan khamis kupitia chama cha ACT-WAZALENDO ameahidi kutoa ushirikiano kwa Mheshimiwa Maryam ili kuhakikisha changamoto za wadi yake zinapatiwa ufumbuzi kwa maslahi mapana ya maendeleo ya kisiwa hicho.

Kwa upande wao, wakazi wa Kisiwa Panza wameeleza kufurahishwa na ziara hiyo na kumpongeza Mhe. Maryam kwa uthubutu na moyo wa kujali wananchi, wakisema kitendo cha kufika kisiwani hapo ni ishara ya uongozi bora unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Aidha, wakazi hao wamebainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo uhaba wa vyoo  jambo ambalo ni hatari kubwa kwa maendeleo ya kiafya katika kisiwa hicho, hivyo wamemuomba kuichukua changamoto iyo na kuifanyia kazi kwani takribani nyumba 480 hawana vyoo jambo ambalo linahtarisha afya zao hasa kuelekea kipindi hichi cha mvua za masika.

Hivyo, wamemuomba Mhe. Maryam kuwa kiunganishi chao kwa viongozi wengine, taasisi mbalimbali na Serikali kwa ujumla ili changamoto hizo ziangaliwe na kupatiwa ufumbuzi.