Popular services

MWAKILISHI WA VITI MAALUM PEMBA ASAMBAZA SARE NA VIFAA VYA SHULE KWA WANAFUNZI WA KIJIJI CHA SHAMIANI.

 

Na Nishan Khamis Pamba
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mariam Said Khamisi, amesambaza sare za shule pamoja na vifaa mbalimbali vya skuli kwa wanafunzi wa kijiji cha Shamiani, Pemba, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono elimu na kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mariam amesema msaada huo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa alipopita katika kijiji hicho kusikiliza changamoto za wananchi, hususan katika sekta ya elimu. Ameeleza kuwa yeye ni kiongozi anayependa vitendo zaidi kuliko maneno, na amedhamiria kuhakikisha ahadi anazozitoa kwa wananchi zinatimizwa kwa vitendo.



Amefafanua kuwa zoezi hilo limefanyika kwa ushirikiano wa viongozi wote wa jimbo na mkoa kwa ujumla, akisisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano wa viongozi ni msingi muhimu katika kutatua changamoto za wananchi. Ameahidi kuendelea kushirikiana nao bega kwa bega katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Aidha, Mariam amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na kuwaunga mkono viongozi wakuu wa nchi, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akisema uongozi wao umeleta kasi kubwa ya maendeleo nchini.