Popular services

UWT YAENZI MAPINDUZI KWA KUSHIRIKI USAFI NA KUTOA SADAKA KITUO CHA AFYA MATEMWE.

 

Na: Nishan Khamis, Matemwe
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Kaskazini A  umetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana katika kudumisha amani, upendo na usafi wa mazingira, sambamba na kuunga mkono juhudi za viongozi wa nchi katika kulinda haiba ya mazingira na kuyafanya yawe kivutio, ikiwa ni msingi wa kuleta maendeleo ya Umoja huo na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Katibu Msaidizi wa UWT Wilaya hiyo Khadija Ali Hamza  wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Matemwe waliposhiriki shughuli za usafi katika Kituo cha Afya cha Matemwe, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Katika tukio hilo, UWT pia ilitoa sadaka kwa wazazi waliokuwepo katika kituo hicho.

Amesema kuwa lengo la shughuli hiyo ni kuendelea kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, akisisitiza kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa. Ameeleza kuwa UWT itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali zote mbili, huku Umoja huo ukiendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kimaendeleo kwa ajili ya jamii na taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa juhudi hizo ni kielelezo cha nafasi kubwa ya wanawake katika uongozi wa mabadiliko nchini, akimtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ni mfano bora wa uongozi thabiti na chachu kwa wanawake viongozi nchini.

Katika hafla hiyo, miongoni mwa sadaka zilizotolewa ni pamoja na sabuni, pampasi, mashuka pamoja na fedha taslim kwa wazazi waliokuwa wakihudumiwa katika Kituo cha Afya cha Matemwe. Aidha, UWT imetoa wito kwa jamii kuendelea kudumisha usafi wa mazingira mara kwa mara na kuunga mkono juhudi za kimaendeleo zinazotekelezwa na viongozi wa nchi.

Kwa upande wao, Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni, Khamis Ali Vuai, na Mwakilishi wa Jimbo hilo, Sulubu Kidongo Amour, wamesema kuwa suala la usafi wa mazingira ni kipaumbele cha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Wamesisitiza kuwa Wilaya hiyo  imezungukwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za utalii, hivyo utunzaji wa mazingira ni jambo muhimu katika kuwavutia watalii na kuongeza pato la taifa.
Hivyo, wamewataka wananchi kuendelea kushirikiana katika kuendeleza utamaduni wa usafi ili kulinda haiba ya maeneo yao, sambamba na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.

Nao wananchi walioshiriki katika zoezi hilo la usafi wametoa pongezi kwa UWT, wakieleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazosababisha uchafuzi wa mazingira katika maeneo yao ni kuachiwa mifugo hovyo. Wamesema hali hiyo husababisha uchafuzi wa mazingira na hivyo kuwaomba viongozi kulishughulikia tatizo hilo ili kuweka mazingira safi na yenye mvuto katika maeneo yao.