Popular services

VIONGOZI WA JIMBO LA MKWAJUNI WAKABIDHI MIPIRA YA MAJI NA TANKI, WANANCHI WATOA PONGEZI

 

Nishan Khamis, Mkwajuni
Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni, Khamis Ali Vuai, amesema ataendelea kutekeleza ahadi kwa vitendo kwa kushirikiana na wenzake na kamati ya siasa jimbo hilo kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali na kutimiza ahadi walizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025.

Ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kukabidhi mipira ya maji katika kijiji cha Uyagu, pamoja na kukabidhi tanki la maji lenye ujazo wa lita 5,000 katika kijiji cha Kibeni.

Aidha, ametembelea shughuli za uchimbaji wa visima vya maji katika shehia za Gamba na Moga. Katika ziara hiyo aliambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Mbunge, Diwani pamoja na Kamati ya Siasa ya Jimbo hilo.


Akizungumza na wananchi wa shehia hizo kwa nyakati tofauti, amesema serikali na viongozi kwa ujumla wana nia njema ya kuwahudumia wananchi kwa kuweka mazingira bora ya miundombinu.

Ameeleza kuwa suala la maji katika Jimbo la Mkwajuni linaendelea kufanyiwa kazi, ambapo serikali inaendelea na ujenzi wa kisima kikubwa cha maji kilichopo Mbuyu Kijungu, hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya maji katika jimbo hilo na wilaya kwa ujumla.

Aidha, amewasisitiza wananchi kuendelea kutunza na kulinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu, sambamba na kuendelea kushirikiana katika kuimarisha maendeleo ya jimbo hilo.

Kwa upande wao, Katibu wa CCM Jimbo la Mkwajuni na Diwani wa Wadi ya Kidombo wamesema utekelezaji huo wa vitendo unatokana na ushindi wa kishindo uliopatikana baada ya wananchi kuichagua CCM. Wamesisitiza kuwa wataendelea kusimamia na kutekeleza Ilani ya chama kwa vitendo, wakieleza kuwa msingi wa maendeleo hayo ni kuendelea kuwaunga mkono viongozi, kutunza amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya jimbo na taifa kwa ujumla.

Nao wananchi wamesema wanashukuru kwa utekelezaji huo wa vitendo, wakieleza kuwa maji ni jambo la msingi na la kwanza katika maisha ya binadamu.

Wamewaomba viongozi hao kuendeleza utamaduni huo wa utekelezaji na kuendelea kushirikiana nao bega kwa bega kwa maendeleo endelevu ya Jimbo la Mkwajuni.