Popular services

DIWANI UNJU AKABIDHI ZAWADI KWA WANAFUNZI WALIOFAULU MICHIPUO SKULI YA KIBUYUNI, AAHIDI KUENDELEZA MAKUBWA.

 Na Nishan Khamis, Kibuyuni

Wazazi na walezi wa kijiji cha Kibuyuni wamehimizwa kuendelea kushirikiana na Kamati za Skuli pamoja na walimu ili kuendeleza maendeleo ya kielimu kwa wanafunzi wa kijiji hicho.

Rai hiyo imetolewa leo na Diwani wa Wadi ya Kidombo, Jimbo la Mkwajuni, Makame Machano Fumu, wakati akizungumza na walimu, Kamati za Skuli pamoja na wanafunzi katika hafla ya ugawaji wa zawadi kwa wanafunzi waliofaulu Darasa la Saba na kuchaguliwa kujiunga na michipuo kutoka Skuli ya Kibuyuni.

Amesema kutokana na mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika katika sekta ya elimu chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, viongozi na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kuunga mkono juhudi hizo pamoja na kutunza miundombinu ya elimu kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Amebainisha kuwa wakati wa kampeni aliahidi kuinua sekta ya elimu katika wadi yake, hivyo utoaji wa mikoba kwa wanafunzi waliofaulu michipuo ni mwanzo tu, akiahidi kuendelea kushirikiana na kuhamasisha maendeleo ya elimu kama kipaumbele katika wadi yake.

Aidha, amewahimiza wazazi, walezi, Kamati za Skuli na walimu kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuleta maendeleo chanya ya kielimu katika skuli hiyo, sambamba na kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini kwani ndio msingi wa maendeleo endelevu.
Awali akizungumza na kumkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Kibuyuni, Mussa Machano Mjomba, amesema ushirikiano kati ya viongozi, Kamati za Skuli na wazazi ni njia bora ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa skuli hiyo.

Ameongeza kuwa ni muhimu wazazi kuwafuatilia watoto wao katika skuli walizopangiwa, kwani kufanya vizuri kwao ni kielelezo chema kwa wanafunzi wengine.

Kwa upande wao, wazazi waliohudhuria hafla hiyo wamempongeza diwani huyo kwa jitihada na ushirikiano mkubwa anaouonyesha katika muda mfupi wa uongozi wake, hasa katika kutatua changamoto za kijamii, jambo linalowapa faraja na matumaini ya kuendeleza maendeleo ya wadi yao.

Nao wanafunzi waliofaulu na kukabidhiwa zawadi hizo wametoa shukrani na pongezi za dhati kwa diwani huyo, wakiahidi kuendelea kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao, sambamba na kumuomba aendelee kuwaunga mkono katika harakati zao za masomo.