Na Nishan Khamis,
Kivunge
Waumini wa dini ya Kiislamu wamekatazwa kusema au kutaja mabaya ya maiti baada ya kutangulia mbele ya haki, kwani kufanya hivyo ni kinyume na mafundisho ya Uislamu na maelekezo ya Mtume Muhammad (s.a.w).
Hayo yameelezwa na Khatibu Ustadh Maulid Salum wakati akitoa hutba ya Swala ya Ijumaa kwa waumini wa Kiislamu waliohudhuria ibada hiyo katika Msikiti wa Muungano uliopo Shehia ya Kivunge, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema katika jamii zetu bado kuna baadhi ya watu wenye tabia ya kutaja au kusema mabaya ya marehemu, jambo ambalo limekatazwa katika Uislamu. Ameeleza kuwa lililo bora na lenye kheri ni kutaja mema ya marehemu, kumuombea dua na kumuachia hukumu Mwenyezi Mungu, kwani kila mmoja wetu ni msafiri wa njia hiyo ya mauti.
Akisisitiza hoja hiyo, Ustadh Maulid Salum amekumbusha hadithi ya Mtume Muhammad (s.a.w) iliyopokewa kutoka kwa Imamu Tirmidhy, inayobainisha kuwa waumini wamekatazwa kutaja mabaya ya maiti na badala yake wahimizwe kutaja mema yao.
Aidha, amekumbusha tukio jingine la Mtume Muhammad (s.a.w) lililosimuliwa na Sahaba Anas bin Malik (r.a), ambapo Mtume alipita pamoja na maswahaba wake karibu na majeneza mawili; jeneza la kwanza liliposifiwa mema alisema “wajibu”, na jeneza la pili liliposemwa mabaya alisema pia “wajibu”, akifafanua kuwa yule aliyesifiwa mema Pepo imemwajibikia, na yule aliyesemwa mabaya Moto umemwajibikia, kama ilivyopokewa pia na Maimamu Bukhari na Muslim.
Halikadhalika, amewasisitiza waumini kuendelea kujiepusha na tabia ya kusemana mabaya, badala yake waamrishane mema na kukatazana maovu, akibainisha kuwa huo ndiyo msingi bora wa kuimarisha mshikamano wa jamii na kufanikisha mafanikio ya maisha ya duniani pamoja na Akhera.
