Popular services

MSTAHIKI MEYA NA MKURUGENZI WAFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA NUNGWI, WALIOKIUKA AGIZO WACHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA.

 

Na Nishan Khamis, Nungwi.
Watu tisa, wakazi wa Nungwi Wilaya ya Kaskazini “A”, wamechukuliwa hatua za kisheria baada ya kukiuka agizo la Baraza la Manispaa la kusitisha ujenzi wa Hoteli ya ZMK iliyopo Nungwi hadi taratibu zote za kisheria zitakapokamilika.

Hatua hiyo imechukuliwa leo kufuatia ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Baraza la Manispaa kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani, ambapo walifika katika eneo la ujenzi na kukuta shughuli za ujenzi zikiendelea licha ya kutolewa kwa maagizo mara tatu ya kusitisha ujenzi huo.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Adam Makame Haji, amesema baraza limesikitishwa na kitendo cha kukaidi maelekezo halali ya mamlaka husika, jambo lililolazimu kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya wahusika wote waliokiuka agizo hilo.

Amesema hatua hizo zimechukuliwa kwa lengo la kuimarisha utii wa sheria, nidhamu na kufuata taratibu za nchi, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu au taasisi iliyo juu ya sheria. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya ujenzi, sambamba na kutoa ushirikiano kwa uongozi wa Manispaa ili kufanikisha maendeleo endelevu katika wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Baraza la Manispaa, Nyange Kher Ali, amesema ziara hiyo ni sehemu ya mikakati ya baraza katika kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa shughuli za maendeleo.
Ameeleza kuwa Nungwi ni eneo muhimu la utalii, na kuendelea kwa ujenzi huo kinyume na sheria kumesababisha usumbufu kwa wageni waliopo katika eneo hilo. Ameongeza kuwa licha ya baraza kutoa agizo rasmi la kusitisha ujenzi, wahusika waliendelea kukaidi maelekezo hayo, hali iliyopelekea sheria kuchukua mkondo wake kwa mujibu wa taratibu zilizopo.