Popular services

ZIARA YA KUSHTUKIZA YA DIWANI UNJU SKULI ZA KIBENI NA MKWAJUNI, WAZAZI NA WALIMU WAMPONGEZA.

 

Na, Nishan Khamis, Mkwajuni
Diwani wa Wadi ya Kidombo, Jimbo la Mkwajuni, Makame Machano Fumu maarufu Unju, amefanya ziara ya kushtukiza katika skuli za Kibeni na Mkwajuni, kwa lengo la kujionea hali ya utoaji wa elimu pamoja na kujadili changamoto na maendeleo ya sekta hiyo katika wadi yake.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Diwani Unju amewataka wazazi, walezi, kamati za skuli na walimu kushirikiana kwa karibu katika kusimamia maendeleo ya elimu, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni msingi muhimu wa kuongeza ufaulu na nidhamu kwa wanafunzi.

Amesema jitihada kubwa zinaendelea kufanywa na viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu, hivyo ni wajibu wa jamii kuziunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha wanafunzi wanasimamiwa ipasavyo.

Aidha, Diwani huyo amewahamasisha wazazi na walezi kuhakikisha wanawaandikisha watoto skuli kwa wakati, akibainisha kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto na ndiyo hazina bora kwa maisha na maendeleo ya baadaye ya mtoto.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walimu katika skuli hizo wamesema ziara ya Diwani imewapa hamasa mpya ya kufanya kazi kwa bidii zaidi, huku wakieleza kuwa ushirikiano mzuri kati ya wazazi, walimu na kamati za skuli umeanza kuleta matokeo chanya katika kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Kwa upande wao, wazazi wamepongeza ziara hiyo ya kushtukiza, wakisema imeonesha dhamira ya dhati ya uongozi wa wadi katika kusimamia maendeleo ya elimu, na wameahidi kuendelea kushirikiana na walimu pamoja na uongozi wa skuli kwa lengo la kuimarisha elimu kwa watoto wao.

Ziara hiyo imetajwa kuwa na matumaini makubwa ya kuimarisha mshikamano kati ya wadau wa elimu na kuleta maendeleo endelevu ya elimu katika wadi ya Kidombo, Jimbo la Mkwajuni kwa ujumla.