Popular services

TAASISI YA JANNAH NA ENSAR DERNEĞI ZATOA MSAADA WA BOTI, WHEELCHAIR NA VYAKULA TUMBATU JONGOWE

 

Na Nishan Khamis – Tumbatu
Taasisi ya Jannah Humanitarian Foundation kwa kushirikiana na Ensar Derneği kutoka nchini Uturuki, imekabidhi msaada wa vyakula, wheelchair pamoja na boti kwa wananchi wa kijiji cha Jongowe, kisiwa cha Tumbatu, wilaya ndogo ya Tumbatu, mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Jannah Humanitarian Foundation, Mohammed Ramadhan Nalyesa, amesema msaada huo ni utekelezaji wa ahadi waliyoitoa baada ya kufanya utafiti katika kisiwa hicho. Amesema kuwa kwa rehema za Mwenyezi Mungu wamefanikiwa kuwapatia msaada huo unaojumuisha vyakula kwa wazee na watu wenye mahitaji maalumu 100, wheelchair 10 pamoja na boti moja kwa ajili ya kusaidia shughuli za kijamii na kiuchumi za kijiji hicho.

Ameeleza kuwa msaada huo hautokani na utajiri wao bali ni tawfiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kuwaomba wananchi waendelee kuwaombea dua ili waweze kuendelea kushirikiana na kuleta misaada mbalimbali katika kisiwa hicho kwa lengo la kutafuta radhi na rehema za Mwenyezi Mungu.

Aidha, ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Ofisi ya Rais, Asma Mwinyi Foundation, pamoja na wakaazi wa kisiwa hicho wakiongozwa na Sheha wa Shehia husika, kwa mapokezi mazuri, ushirikiano na muitikio mkubwa waliouonesha katika hafla hiyo.
Kwa upande wake, Sheha wa Shehia hiyo, Ali Khamis Silima, amesema taasisi hiyo ilifika kijijini hapo wiki mbili zilizopita kwa ajili ya kufanya utafiti na kuahidi kutoa msaada wa vyakula, wheelchair pamoja na boti, ahadi ambayo ameipongeza kwa kutekelezwa kwa muda mfupi. Amewaomba kuendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya kisiwa hicho.

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamesema wanashukuru kwa msaada huo ambao utawasaidia kwa kiasi kikubwa, na kuwaomba wafadhili hao kuendelea kuwasaidia katika harakati nyingine za kijamii, hususan masuala ya utunzaji wa mazingira katika kisiwa hicho