Popular services

MHE. MARIAM SAID KHAMIS AIBUA TABASAMU KWA WAJASIRIAMALI CHAKE CHAKE KWA KUKABIDHI VYARAHANI NA FEDHA TASLIM

 

Nishan Khamis, Pemba
Mheshimiwa Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Mariam Said Khamis, ameendeleza utekelezaji wa ahadi zake kwa vitendo kwa kuwasaidia wajasiriamali wadogo wa ushonaji kutoka Shehia ya Chake Chake Madungu, Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni ahadi aliyotoa katika kipindi cha kampeni tukio hilo likiendana na shamra shamra za kutimiza miaka 49 ya Kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Mariam amesema msaada huo unatokana na jitihada kubwa zinazofanywa na wajasiriamali hao, hususan mchango wao katika kushughulikia ushonaji wa nguo za Chama Cha Mapinduzi wakati wa kampeni, hatua inayolenga kuwaongezea kasi ya kujiinua kiuchumi kupitia shughuli zao za ujasiriamali.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Mheshimiwa Mariam amekabidhi mashine mbili za kisasa za ushonaji zenye thamani ya shilingi laki tisa pamoja na fedha taslim kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali. Amesisitiza kuwa ataendelea kuwaunga mkono bega kwa bega na kutoa wito kwa wadau mbalimbali na viongozi kuendelea kuwaunga mkono wajasiriamali wanawake na jamii kwa ujumla ili kuinua uchumi wao.

Aidha, hafla hiyo imefanyika sambamba na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametajwa kuwa ni kiongozi wa mfano wa mwanamke kutokana na umakini na weledi wake katika kusimamia maendeleo ya nchi.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa UWT Jimbo la Chake Chake, Maua Bedui Hamad, amempongeza Mheshimiwa Mwakilishi kwa kuwajali na kuwaunga mkono wajasiriamali hao, akisema ni mfano bora wa kiongozi anayethamini wananchi wake na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wao, wajasiriamali hao wameshukuru kwa msaada walioupata wakisema ni hitaji muhimu katika shughuli zao, ambao utakuwa chachu ya kuongeza uzalishaji na pato la uchumi wao.

Wamempongeza Mheshimiwa Mwakilishi wa Viti Maalum na kumuahidi kutunza rasilimali walizopatiwa ili zidumu kwa muda mrefu kwa maslahi mapana ya kujiinua kiuchumi.