Popular services

MWAKILISHI WA VITI MAALUM MKOA WA KUSINI PEMBA, MARYAM SAID KHAMIS, AENDELEZA ZIARA ZA KUSIKILIZA KERO NA CHANGAMOTO ZA WANAWAKE KATIKA SHEHIA ZA UWELENI NA MAPINDUZI

 

Na, Nishan Khamis, Pemba.
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Mheshimiwa Maryam Said Khamis, ameendeleza ziara zake za kikazi katika shehia za Uweleni na Mapinduzi kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wanawake pamoja na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.

Ziara hizo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono sera na mipango ya maendeleo inayotekelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, kwa kuhakikisha wananchi wananufaika na maendeleo yanayotekelezwa.

Katika ziara yake, Mheshimiwa Maryam amepata fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake, hususan katika upatikanaji wa huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi.

Miongoni mwa changamoto zilizobainika ni uhaba wa umeme katika baadhi ya maeneo yasiyo rafiki, hali inayokwamisha shughuli za kila siku za wanawake. Mheshimiwa Maryam ameahidi kushirikiana na taasisi husika ili kuweka taa na kuboresha mazingira ya usalama na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Aidha, katika wadi ya Napia, Mheshimiwa Maryam ameahidi kusaidia upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa kupeleka mipira ya maji katika maeneo yenye uhitaji mkubwa. Pia ameahidi kuendelea kutoa msaada kwa kina mama wa Madrasa pamoja na jamii kwa ujumla, ili kuwawezesha kupata fursa zaidi za maendeleo na ustawi wa kijamii.

Ziara hizi zinaonesha dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Maryam Said Khamis ya kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kusikiliza wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa vitendo, huku akisisitiza mshikamano na ushirikiano katika kuleta maendeleo endelevu Mkoa wa Kusini Pemba.

Kwa upande wao, wananchi wa shehia za Uweleni na Mapinduzi wamempongeza Mheshimiwa Maryam kwa juhudi zake na kumuomba kuendelea kushughulikia changamoto za kijamii zinazowakabili wanawake ili kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.