Popular services

DIWANI UNJU AHIDI KUCHANGIA MCHANGA NA MAWE UJENZI WA DARASA SKULI YA MSINGI KIBENI,AKABIDHIZAWADIKWAWANAFUNZIWALIOFAULUMICHIPUOKIBENI. .

 

Na Nishan Khamis, Kibeni
Wakaazi wa kijiji cha Kibeni, Wilaya ya Kaskazini “A”, wametakiwa kushirikiana katika ujenzi wa darasa moja na ukumbi wa mikutano katika Skuli ya Msingi Kibeni, kufuatia ongezeko la idadi ya wanafunzi katika skuli hiyo.

Wito huo umetolewa na Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi na Sekondari Kibeni, Haji Mtumwa Ame, wakati akizungumza katika kikao cha wazazi, walezi na Kamati ya Skuli ya Kibeni kilicholenga kujadili changamoto zinazoikabili skuli hiyo pamoja na harakati za kuanza ujenzi wa miundombinu mipya ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Aidha, Mwalimu Mkuu huyo alitoa pongezi za dhati kwa Diwani wa Wadi ya Kidombo kwa ushiriki wake mkubwa na ushirikiano anaouonesha katika kusukuma mbele maendeleo ya skuli hiyo pamoja na wadi kwa ujumla.

Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Wadi ya Kidombo, Makame Machano Foum, aliwahakikishia wazazi, kamati ya skuli na walimu kuwa atashirikiana nao kikamilifu katika ujenzi wa darasa na ukumbi wa mikutano. Aliahidi kuanza kwa kuchangia magari manne ya mawe na gari moja la mchanga, na kusisitiza kuwa ataendelea kushirikiana nao hadi ujenzi huo utakapokamilika.

Kwa lengo la kuwahamasisha wanafunzi, Diwani huyo aliwakabidhi zawadi za mabegi ya skuli wanafunzi wote waliofaulu mitihani ya michipuo kutoka skuli hiyo, sambamba na kutoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana katika kuendeleza maendeleo ya skuli na wadi kwa ujumla.
Kwa upande wao, wananchi waliohudhuria kikao hicho walisema kutokana na ongezeko la watoto ni muhimu kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Pia walitoa pongezi za dhati kwa Diwani kwa ukaribu wake na wananchi, moyo wa kujali na juhudi zake za kushughulikia changamoto za jamii katika wadi hiyo, hali ambayo imewapa faraja na matumaini. Walitoa wito kwa viongozi wengine kuiga mfano huo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya jamii.