Na: Nishan Khamis, Matemwe
Mkuu wa Kituo cha Afya cha Matemwe, Dkt. Rabia Kasimu Mohamed, amesema ukosefu wa uzio katika kituo hicho unachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, hali inayohatarisha afya za binadamu.
Ameeleza kuwa kituo hicho pia kinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi, jambo linaloathiri usafi wa mazingira na utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa.
Aidha, amesema ukosefu wa jenereta pamoja na gari la kubebea wagonjwa (ambulance) ni changamoto kubwa inayosababisha usumbufu katika kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma za haraka.
Kwa upande wake, Juma Ahmada Ali, Mkuu wa Huduma za Mama na Mtoto katika kituo hicho, amesema anaishukuru Serikali kwa ujenzi wa jengo zuri la huduma za Mama na Mtoto.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya maji, umeme, ambulance pamoja na kukosekana kwa dereva, hali inayopunguza ufanisi wa huduma zinazotolewa.
Kutokana na changamoto hizo, ameiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kusaidia kutatua changamoto hizo kwa maslahi mapana ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa kijiji cha Matemwe.
Naye, Mratibu wa Huduma za Afya Wilaya ya Kaskazini A, Rajab Khamis Rajab, amesema bado kuna baadhi ya changamoto nyingi katika hospitali na vituo vya afya wilayani humo, lakini Serikali inaendelea kuchukua hatua kwa kufanya tathmini na tafiti ili kupata suluhisho la kudumu.
Kwa upande wao, Mbunge wa Jimbo la Mkwajuni, Khamis Ali Vuai, pamoja na Mwakilishi wa Jimbo hilo, Sulubu Kidongo Amour, wameahidi kununua jenereta ili kusaidia kutatua changamoto ya umeme katika Kituo cha Afya cha Matemwe.
