Na: Nishan Khamis, Potoa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, hatua inayokwenda sambamba na maboresho ya mitaala pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kisasa ikiwemo majengo ya shule na vifaa vya kujifunzia.
Dkt. Mkuya ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Shule ya Msingi Potoa, itakayohudumia wanafunzi kutoka shule za Msingi Mwera Mtofaani na Vuga Mkadini. Ufunguzi huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mtoto kielimu hayawezi kupatikana kwa juhudi za Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na walimu katika kusimamia na kufuatilia maendeleo ya watoto wao ili kuhakikisha miundombinu iliyowekwa inaleta matokeo chanya katika ufaulu wa wanafunzi.
Aidha, Dkt. Mkuya amesema Serikali imetumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu hiyo, hivyo ni wajibu wa jamii kwa pamoja kuitunza ili iweze kutumika kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Potoa pamoja na shule za Mwera Mtofaani na Vuga Mkadini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Amos John Henok, amesema ujenzi wa shule hizo ulianza rasmi mwezi Septemba 2024 na kukamilika Desemba 2025.
Amesema mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 6 na utachukua zaidi ya wanafunzi 1,000, kwa wastani wa wanafunzi 45 kwa kila darasa, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa wanafunzi pamoja na kupunguza masafa marefu wanayosafiri kwenda shule.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Rashid Simai Msaraka, amesema maboresho ya sekta ya elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, yakilenga kuwajengea vijana uwezo wa kupata elimu bora, taaluma, ufanisi na umakini wa kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar kwa vizazi vijavyo.

