Na Nishan Khamis, Gamba
Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, ameendelea kutekeleza ahadi yake kwa vitendo baada ya kuchangia mifuko 100 ya saruji, malori mawili ya mchanga pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Kaskazini A.
Mhe. Ayoub ametoa mchango huo wakati akizungumza na wanachama wa UWT Wilaya ya Kaskazini A katika makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, yaliyopo Gamba. Amesema kuwa uimarishaji wa jumuiya za chama ni jambo la msingi, huku akisisitiza utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya CCM kama nguzo muhimu ya maendeleo ya UWT na chama kwa ujumla.
Aidha, amesema umoja na mshikamano uliopo miongoni mwa wanachama wa UWT ni chachu ya maendeleo, na kuwataka kuendelea kubuni na kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali kwa lengo la kuimarisha uchumi wa jumuiya kwa maslahi yao, chama na jamii kwa ujumla. Pia amewasisitiza kuendelea kuwaombea dua viongozi wakuu wa nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ili waendelee kuiongoza nchi katika misingi imara ya maendeleo.
Kwa upande wake, Katibu wa UWT Wilaya ya Kaskazini A, Mtenge Makame Faki, amesema mchango uliotolewa na Mhe. Ayoub ni chachu kubwa ya kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hiyo. Ametoa pongezi za dhati kwa Mbunge huyo kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi aliyotoa katika Mkutano Mkuu wa UWT wa wilaya hiyo.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mama Chatanda, aliyesisitiza kila wilaya kuwa na nyumba maalum ya Katibu wa UWT ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa jumuiya. Aidha, amesema kwa ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa UWT wilaya hiyo, watahakikisha jengo hilo linakamilika kwa wakati ili kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo.
Nao, baadhi ya wajumbe wa Kamati Tendaji ya UWT Wilaya ya Kaskazini A wametoa pongezi zao kwa Mhe. Ayoub kwa msaada mkubwa alioutoa, wakieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo ni hatua muhimu ya maendeleo kwa jumuiya hiyo. Pia wamewaomba viongozi wengine kuendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuendeleza maendeleo ya CCM wilaya na taifa kwa ujumla.


