Popular services

MHE, HEMED AZINDUA HOTEL YA MATEMWE ATTITUDE,UWEKEZAJI WA UTALII WAIMARISHA AJIRA NA UCHUMI ZANZIBAR.

 

Na Nishan Khamis, Matemwe
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Sekta Binafsi itaendelea kuhakikisha Sekta ya Uwekezaji inazidi kukua na kuimarika zaidi nchini.

Mhe. Hemed ameyasema hayo katika uzinduzi wa mradi wa hoteli ya Matemwe Attitude iliyopo Kijini, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuimarika kwa sekta ya uwekezaji ndiko kunakowavutia wawekezaji kuendelea kuwekeza kwa wingi Zanzibar, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa ajira kwa wananchi wazawa pamoja na kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka maeneo ya uwekezaji.

Amefahamisha kuwa jitihada hizo zimezaa matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo Utalii, Ujenzi na Nishati, hali iliyosababisha kupatikana kwa fursa nyingi za ajira. Takwimu za Serikali zinaonesha kuwa zaidi ya miradi 588 ya uwekezaji imesajiliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 6.9 na kuweza kuzalisha ajira zaidi ya 28,695 kwa wazawa.

Mhe. Hemed amesema amefurahishwa na kauli ya mwekezaji wa Hoteli ya Matemwe Attitude ya kuahidi kuweka kipaumbele katika kuboresha mazingira yanayowazunguka sambamba na kuigusa jamii moja kwa moja katika nyanja mbalimbali, lengo likiwa ni kuhakikisha ustawi bora wa wananchi wa Kijini na Mkoa wa Kaskazini kwa ujumla.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji ili waendelee kuja kuwekeza Zanzibar, huku akiwahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na kulinda mila, silka na tamaduni za Kizanzibari.

Sambamba na hayo, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano, kulinda, kudumisha na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ili kuendelea kupata maendeleo endelevu nchini.


Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Hoteli ya Matemwe Attitude, Bw. Ravin Unthiah, amesema wameamua kuwekeza Zanzibar kutokana na amani na utulivu uliopo, mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na ushirikiano mkubwa unaotolewa na wananchi, hali inayofanya mazingira ya uwekezaji kuwa rafiki na wezeshi.

Amefahamisha kuwa uzinduzi wa hoteli hiyo utatoa fursa za ajira zaidi ya 190 kwa wananchi wa Kijini na Mkoa wa Kaskazini kwa ujumla, ambapo wafanyakazi hao tayari wamepatiwa mafunzo na ujuzi kulingana na kada zao ili waweze kutoa huduma bora kwa wageni na wazawa watakaotembelea hoteli hiyo.

Ameongeza kuwa Matemwe Attitude Group ina zaidi ya hoteli tisa (9) zenye madaraja tofauti, na kwamba pamoja na uwekezaji huo, kwa kushirikiana na Serikali, kundi hilo limejipanga kusaidia kukuza uchumi na kuisaidia jamii inayowazunguka katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Akitoa salamu za Mkoa Mkuu wa Mkoa huo, Cassian Gallos Nyimbo, amesema kupitia Serikali inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, mkoa huo umeendelea kuwa kivutio kikubwa cha wawekezaji. Amesema Serikali imejidhatiti katika kuondoa changamoto za maji, umeme na ajira kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Mkoa huo na Zanzibar kwa ujumla.