Popular services

MWAKILISHI WA VITI MAALUM MKOA WA KUSINI PEMBA, MARYAM SAID KHAMIS, AENDELEZA ZIARA ZA KUSIKILIZA CHANGAMOTO ZA WANAWAKE SHEHIA YA KIBOKONI.

 

Na: Nishan Khamis, Pemba
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Mheshimiwa Maryam Said Khamis, leo ameendeleza ziara zake za kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake wa Shehia ya Kibokoni, iliyopo Jimbo la Wawi, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni shamra shamra za kutimiza miaka 49  ya chama cha mapinduzi.

Akizungumza na wanawake hao, Mheshimiwa Maryam amesema lengo la ziara hiyo ni kusikiliza changamoto zao ili zile anazoweza kuzitatua yeye mwenyewe azifanyie kazi, huku changamoto kubwa zaidi akiahidi kuzikabidhi kwa viongozi wa jimbo hilo kwa ushirikiano, na nyingine kuziwasilisha Serikalini kwa ufumbuzi wa kudumu.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Maryam kwa kuonesha utayari wa vitendo, alikabidhi fedha taslim kwa ajili ya utatuzi wa changamoto ya vifaa vya maji katika baadhi ya maeneo ya shehia hiyo sambamba kuwaahidi kutatuachangamoto zingine zilizopo katika uwezowake.

Aidha, aliwasihi wanawake hao kuendelea kuwa wamoja, kushirikiana katika shughuli za maendeleo, pamoja na kuwaombea dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili waendelee kuwa na afya njema na kuiongoza nchi kwa maendeleo zaidi.

Wakieleza changamoto zao, wanawake wa Shehia ya Kibokoni wamesema tatizo la maji ni changamoto kubwa inayowasababishia usumbufu mkubwa katika maisha yao ya kila siku. Pia wametaja ukosefu wa uwezeshaji wa mikopo kwa wajasiriamali pamoja na ukosefu wa ajira kwa watoto wao, hali inayochangia baadhi ya vijana kujiingiza katika vitendo vya wizi katika kijiji hicho.

Aidha, wametoa pongezi za dhati kwa Mwakilishi huyo wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba kwa uthubutu wake wa kufika kijijini hapo na kusikiliza kero na changamoto zao, wakisema ni mara ya kwanza kwa kiongozi kufika na kufanya hivyo katika jimbo hilo. Wanawake hao wamesema hatua hiyo imewapa matumaini mapya na kuonesha muelekeo mzuri wa uongozi unaowajali na kuwatumikia wananchi, hususan wanawake, katika kuleta maendeleo.