Popular services

DIWANI UNJU AAMUA KUVUNJA KIKWAZO CHA USAFIRI MICHEZONI, VIJANA WA KIDOMBO WAMPA MAU YAKE.

 

Na Nishan Khamis, Mkwajuni

Diwani wa Wadi ya Kidombo, Jimbo la Mkwajuni, Makame Machano Fumu maarufu Unju, ameamua kuvunja kikwazo cha usafiri kwa vijana wanaojihusisha na michezo katika wadi hiyo, hatua inayolenga kukuza vipaji vyao na kuwapa fursa ya kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya eneo lao.

Diwani Unju ameyasema hayo leo wakati akizungumza na vijana wa timu ya mpira wa miguu ya Eleven Boys kutoka Shingwi, ambapo amesema atakuwa bega kwa bega na vijana katika harakati zote za michezo, ikiwemo kuwasaidia pale changamoto ya usafiri inapojitokeza, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikirejesha nyuma maendeleo ya michezo katika wadi ya Kidombo.



Amesema dhamira yake ni kuona vijana wanatumia michezo kama fursa ya ajira, kujipatia kipato na kuitangaza wadi pamoja na taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya maendeleo na kujenga afya bora kwa jamii.
Aidha, Diwani Unju amewahimiza vijana kuzingatia nidhamu, mshikamano na kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na utulivu wa nchi, sambamba na kuendeleza vipaji vyao vya michezo.

Kwa upande wao, vijana wa Kidombo wameonyesha furaha na kumpongeza Diwani Unju kwa hatua na juhudi anazochukua tangu aingie madarakani, wakieleza kuwa amekuwa mstari wa mbele katika kuwapatia misaada na sapoti mbalimbali katika shughuli za michezo.

Nahodha wa timu ya Eleven Boys, Haruna Khamis Kibaden, amesema wanajivunia kuwa na kiongozi anayejali michezo katika wadi yao, na wamemuahidi kuendelea kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa ili kufikia malengo ya maendeleo ya timu, wadi na taifa kwa ujumla.