Popular services

DIWANI UNJU ATEKELEZA AHADI YA KUBORESHA BANDA LA WAJASIRIAMALI WANAWAKE KIBENI

 

Na Nishan Khamis, Kibeni
Diwani wa Wadi ya Kidombo, Makame Machano Fumu maarufu Unju, leo ametekeleza kwa vitendo ahadi yake ya kupeleka kifusi na kuboresha banda la wajasiriamali wadogo wadogo wanawake lililopo katika Skuli ya Kibeni, Jimbo la Mkwajuni, Wadi ya Kidombo, Wilaya ya Kaskazini “A”.

Akizungumza katika tukio hilo, Diwani Unju amesema lengo lake ni kuhakikisha wananchi wa wadi hiyo, hususan wanawake wajasiriamali wadogo wadogo, wanakuwa na mazingira rafiki ya kufanya biashara zao ili wawe salama na huru zaidi katika kujipatia kipato kupitia shughuli wanazozifanya. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kumuinua mwanamke kiuchumi.

Ameeleza kuwa uamuzi wa kupeleka kifusi na kuboresha eneo hilo kwa kiwango bora ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa wakati wa kampeni, na sasa ni wakati muafaka wa kutekeleza kwa vitendo yale yote aliyoyaahidi, hatua kwa hatua, ili Wadi ya Kidombo iwe mfano wa maendeleo katika wilaya na mkoa kwa ujumla.

Aidha, amewasisitiza wajasiriamali hao kuendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi za viongozi katika kuleta maendeleo, sambamba na kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri na kutunza amani na utulivu nchini.

Akipokea kifusi hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Kibeni, Mussa Haji Makame, amempongeza Diwani huyo kwa kuwa mkweli wa ahadi na kwa utekelezaji wake wa vitendo. Amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa na kumuomba aendelee na moyo huo, kwani ukarabati wa eneo hilo utawasaidia kwa kiasi kikubwa wajasiriamali hao kuwa salama kiafya na kimazingira.

Hivyo, amemhakikishia Diwani Unju kuendelea kushirikiana naye bega kwa bega katika harakati mbalimbali za kimaendeleo ndani ya skuli hiyo na Wadi ya Kidombo kwa ujumla, ili kutatua changamoto zilizopo.