Na Nishan Khamis, Mkwajuni.
Jumatano,07,2026.
Walimu wakuu wa Wilaya ya Kaskazini “A” wametakiwa kushirikiana kwa karibu na jamii katika suala la uandikishaji wa watoto shule, sambamba na kusimamia kwa umakini tabia za baadhi ya walimu wenye changamoto ya utoro, uchelewaji wa kufika shuleni pamoja na kuwahi kuondoka kabla ya muda rasmi wa kazi.
Wito huo umetolewa na Afisa Elimu wa Wilaya ya Kaskazini “A”, Juma Mwadin Abdalla, alipokuwa akizungumza na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Walimu Mkwajuni wilaya hiyo.
Amesema walimu wakuu wana jukumu la msingi la kusimamia kwa karibu utendaji wa walimu waliopo chini yao, bila kuacha mambo ya muhali, ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa maslahi mapana ya elimu ya vijana, wilaya na taifa kwa ujumla.
Aidha, Afisa Elimu huyo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya walimu wakuu, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla, akieleza kuwa ushirikiano huo ni nguzo muhimu katika kutatua changamoto za elimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Vilevile, amehimiza kuwepo kwa vikao vya mara kwa mara baina ya walimu wakuu na walimu wa shule zao, akibainisha kuwa vikao hivyo ni njia bora ya kusikiliza changamoto, kubadilishana mawazo na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha maendeleo ya wanafunzi na walimu, jambo litakalochangia ongezeko la ufaulu. Pia ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya shule za serikali na binafsi katika kuendeleza sekta ya elimu ndani ya wilaya hiyo.
Kadhalika, amewataka walimu kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuimarisha sekta ya elimu, juhudi ambazo amesema zimeleta mageuzi makubwa ya kielimu katika wilaya hiyo. Sambamba na hilo, amewapongeza walimu kwa usimamizi mzuri uliosababisha matokeo mazuri ya mtihani wa Darasa la Saba, na kuwataka kuongeza bidii ili Wilaya ya Kaskazini “A” iendelee kufanya vizuri zaidi kitaifa.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Taaluma Msingi wa wilaya hiyo, Mgeni Juma Rashid, amesisitiza walimu wakuu kuendelea kusimamia ipasavyo suala la usafi wa wanafunzi na mazingira ya shule, akieleza kuwa uangalizi wa afya ni jambo muhimu katika kudhibiti magonjwa mbalimbali yanayoweza kuathiri mahudhurio na ufaulu wa wanafunzi.
Nao walimu wakuu walioshiriki kikao hicho wamesema kuwa mkutano huo ni muendelezo mzuri wa kuimarisha ushirikiano na uwajibikaji katika kuleta maendeleo chanya ya elimu, na kuahidi kuyachukua na kuyafanyia kazi yote yaliyojadiliwa kwa lengo la kuendeleza gurudumu la maendeleo ya elimu katika Wilaya ya Kaskazini “A”.


