Popular services

SHEHA WA MATEMWE KIGOMANI AUNGANA NA WATALII KUADHIMISHA MAPINDUZI KWA USAFI.

 

Na: Nishan Khamis, Matemwe.
Sheha wa Shehia ya Matemwe Kigomani, Juma Simai Juma, amewahimiza wanakijiji hicho kuendeleza utamaduni wa kushirikiana katika shughuli za usafi wa mazingira na masuala mbalimbali ya kijamii, ili kutatua changamoto zilizopo pamoja na kuweka haiba nzuri inayovutia katika fukwe na maeneo yote ya kijiji hicho.

Sheha Juma ameyasema hayo leo huko Kigomani, wakati wa zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo ya fukwe, ambapo alijumuika na taasisi mbalimbali, watalii pamoja na wanakijiji, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa Matemwe ni eneo la kitalii, hivyo kuendelea kuweka mazingira safi mara kwa mara ni kivutio kikubwa kwa watalii, sambamba na kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuimarisha uwekezaji wa mazingira safi na yenye mvuto visiwani Zanzibar.
Qq
Aidha, ametoa wito kwa jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii, sambamba na kudumisha amani na utulivu nchini.

Akizungumza katika zoezi hilo, Othman Omar Othman kutoka taasisi ya Under The Wave, inayojihusisha na uhifadhi wa bahari na fukwe zake, amesema anamshukuru na kumpongeza Sheha wa Shehia hiyo kwa ushirikiano mzuri pamoja na kuishirikisha taasisi hiyo katika zoezi hilo. Ameshauri shughuli hizo ziwe endelevu ili kudumisha usafi wa fukwe na mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wao, watalii na wanakijiji wa Matemwe wametoa pongezi za dhati kwa Sheha kwa kuandaa zoezi hilo kwa ushirikiano mkubwa, huku wakitoa wito kwa jamii ya kijiji hicho kujenga utamaduni wa kushiriki katika harakati mbalimbali za kijamii.